Michezo

Kiwango cha soka cha Harambee Stars chasalia chini

September 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

HARAMBEE Stars wamepanda kwa nafasi moja zaidi kutoka nambari 107 hadi 106 kwenye orodha ya viwango bora vya kimataifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) mnamo Septemba 17, 2020.

Hata hivyo, timu ya taifa ya wanawake almaarufu Harambee Starlets wameteremka kwa nafasi nne zaidi kutoka 133 hadi 137 kimataifa.

Licha ya kutoshiriki mchuano wowote kwa kipindi cha miezi kadhaa iliyopita kutokana na janga la corona, kupanda kwa Harambee Stars, japo kwa kiasi kidogo, kumemfurahisha sana kocha Francis Kimanzi.

“Hizi ni habari za kutia moyo sana. Zinakuja wakati ambapo tunajiandaa kwa mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) zitakazondaliwa nchini Cameroon,” akasema Kimanzi kwa kusisitiza kwamba msimamo wao kimataifa pia ni changamoto kubwa kwa Stars kujitahidi hata zaidi kuimarika kwenye orodha hiyo.

“Tulifanya vyema kabla ya mkurupuko wa virusi vya corona. Janga hili limevuruga maandalizi yetu. Hata hivyo, tunasubiri mwongozo utakaotolewa na serikali ili tujue namna ya kujifua vilivyo kwa kampeni zilizopo mbele yetu,” akaongeza Kimanzi.

Kenya kwa sasa inashikilia nafasi ya pili kwenye Kundi G la kufuzu kwa AFCON 2021. Stars wanajivunia alama mbili kutokana na sare za 1-1 dhidi ya Misri ugenini na Togo nyumbani. Mchuano ujao utawakutanisha na Comoros jijini nyumbani na ugenini mnamo Novemba 9 na 12 mtawalia.

Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) tayari limefichua mipango ya kuwajibisha Stars katika mechi mbili za kirafiki mnamo Oktoba. Mojawapo ya mechi hizo za kupimana nguvu itakuwa dhidi ya Sudan.

Ubelgiji wangali kileleni mwa orodha ya FIFA wakifuatwa na Ufaransa, Brazil na Uingereza. Barani Afrika, Senegal wanaongoa wakifuatwa na Tunisia, Nigeria na Algeria.