• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Kizungumkuti cha Oezil baada ya Arsenal kumtema kwenye kikosi cha Europa League 2020-21

Kizungumkuti cha Oezil baada ya Arsenal kumtema kwenye kikosi cha Europa League 2020-21

Na MASHIRIKA

KIUNGO Mesut Oezil hajajumuishwa kwenye kikosi cha wanasoka 25 kitakachotegemewa na Arsenal kwenye kampeni za Europa League msimu huu wa 2020-21.

Nyota huyo mzaliwa wa Uturuki na raia wa Ujerumani huenda pia akakosa kuunga orodha ya wachezaji watakaochezea Arsenal kwenye mapambano ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na Kombe la FA msimu huu.

Chini ya mkufunzi Mikel Arteta, Arsenal wana siku 10 pekee kupokeza vinara wa EPL na wasimamizi wa Shirikisho la Soka la Uingereza (FA) orodha kamili ya wachezaji watakaowajibishwa kwenye mapambano hayo muhula huu.

Sh49 milioni ambazo Oezil kwa sasa kwa wiki uwanjani Emirates zinamfanya kuwa mwanasoka ghali zaidi anayedumishwa kimshahara kambini mwa Arsenal.

Kuachwa nje kwa Oezil katika kikosi kitakachoshiriki soka ya Europa League kunaashiria kwamba huenda sogora huyo wa zamani wa Real Madrid akawa amechezea Arsenal mchuano wake wa mwisho licha ya kwamba angali na miezi minane kwenye mkataba wake na kikosi hicho.

Orodha ya kikosi kitakachotegemewa na Arsenal kwenye Europa League iliwasilishwa kwa Shirikisho la Soka la bara Ulaya (Uefa) mnamo Oktoba 7, 2020, siku moja baada ya Ozil kujitolea kugharimia mshahara wa Jerry Quy ambaye amekuwa akitumika kama maskoti ya Gunnersaurus uwanjani Emirates kwa kipindi kirefu.

Mnamo Oktoba 5, 2020, Arsenal walifichua kwamba Guy, ambaye amekuwa akiwapa mashabiki na wachezaji burudani ya kipekee uwanjani kwa miaka 27 iliyopita, alikuwa sehemu ya vibarua 55 ambao watafutwa kazi baada ya hazina ya fedha ya Arsenal kulemwazwa na corona.

Hadi kufikia sasa, Arsenal wamejisuka vilivyo na ujio wa Thomas Partey aliyeagana na Atletico Madrid ya Uhispania unatarajiwa kumchochea Ozil kuondoka uwanjani Emirates kabla ya mkataba wake kukamilika rasmi mwishoni mwa Juni 2021.

Partey ambaye ni raia wa Ghana, anatazamiwa sasa kushirikiana vilivyo na Dani Ceballos, Willian Borges, Mohamed Elneny na Granit Xhaka kenye safu ya kati ya Arsenal ambao wameagana na viungo Matteo Guendouzi na Lucas Torreira ambao walitua Hertha Berlin na Atletico mtawalia kwa mkopo.

Zaidi ya kusajili Partey na Willian, Arsenal walijinasia pia huduma za beki Gabriel Magalhaes na kipa Alex Runarsson baada ya kuwapokeza madifenda Pablo Mari na Cedric Soares mikataba ya kudumu mwanzoni mwa kampeni za msimu huu wa 2020-21.

Kwa mujibu wa kanuni za Uefa, kati ya wanasoka 25 ambao vikosi vitalenga kutegemea kwenye kampeni za Europa League, wote wanastahili kuwa na umri wa zaidi ya miaka 21 na angalau wanane kati yao wawe wamesakata soka ya ligi ambayo kikosi husika kinashiriki kwa angalau misimu mmoja.

Ilivyo, Arteta aliamua kumtema Oezil kikosini mwake baada ya Arsenal kushindwa kumpa sogora huyo kitita kikubwa cha ujira anaostahili kupokezwa kwa mujibu wa mkataba wake ili atafute hifadhi mpya kwingineko.

Mechi ya mwisho kwa Oezil kuchezea Arsenal ni ile iliyoshuhudia kikosi hicho cha Arteta kikiwapokeza West Ham United kichapo cha 1-0 ligini mnamo Machi 7, 2020.

Japo Oezil atakuwa akishiriki mazoezi kambini mwa Arsenal, matumaini yake ya pekee ya kusakata soka msimu huu ni kujiunga na kikosi cha Ligi ya Daraja la Kwanza (Championship) kabla ya Oktoba 16 ambayo ni siku ya mwisho ya uhamisho wa wachezaji katika ligi ndogo za soka nchini Uingereza.

Oezil pia ana uhuru wa kuvunja ghafla uhusiano wake na Arsenal na kuingia katika sajili rasmi ya kikosi chochote kisichokuwa cha EPL kabla ya Oktoba 19, 2020 au kuwapa Arsenal barua ya kumruhusu ajiunge na klabu yoyote nyingine barani Ulaya katika muhula mfupi wa uhamisho wa wachezaji mnamo Januari 2021.

You can share this post!

Ureno na Uhispania bado ni nguvu sawa

Vijana wahamasishwe badala ya kutumiwa vibaya – mbunge