KK Homeboyz yapiku Gor, Bandari katika ngazi ya ligi
Na GEOFFREY ANENE
KAKAMEGA Homeboyz imerukia juu ya jedwali la Ligi Kuu ya Soka ya Kenya ambayo imeshuhudia mabadiliko mengi baada ya mechi za raundi ya tatu kusakatwa wikendi.
Baada ya kuzamisha Kariobangi Sharks kwa mabao 3-0 kupitia kwa magoli ya Allan Wanga (mawili) na Ken Onyango uwanjani Bukhungu, Homeboyz imepaa kutoka nafasi ya tatu hadi kileleni mwa ligi hii ya klabu 18 kwa alama saba.
Bandari ni nambari mbili kwa alama sawa, lakini na uhafifu wa magoli baada ya kuimarika nafasi mbili kutokana na ushindi wake wa pili mfululizo ilipobwaga SoNy Sugar 1-0 mjini Awendo. Darius Msagha alipachika bao hilo la pekee.
Mabingwa watetezi Gor Mahia wamepiga hatua tatu mbele hadi nafasi ya tatu. Wamezoa alama sita kutokana na mechi mbili.
Walipepeta KCB 2-1 uwanjani Machakos kupitia mabao ya Mghana Francis Afriyie na Lawrence Juma naye Enock Agwanda akafungia wanabenki hao bao la kufutia machozi.
Washindi wa mwaka 2008 Mathare United wamerukia nambari nne kutoka nafasi ya tisa baada ya kuandikisha ushindi wao wa kwanza dhidi ya Ulinzi Stars tangu mwaka 2016 kwa kuchapa wanajeshi hao 2-1.
Mathare, ambayo ina alama tano, ililemea mabingwa mara nne wa zamani Ulinzi kupitia mabao ya David Owino na Clifford Alwanga. Daniel Waweru alipachika bao la Ulinzi.
Western Stima, ambayo imetoshana na Mathare kila kitu, inashikilia nafasi ya tano kutoka nambari 10 baada ya kuzima Posta Rangers 1-0 mjini Machakos kupitia bao la Villa Oromchan.
Mabingwa wa mwaka 2009 Sofapaka walipepeta Chemelil Sugar 4-0 kupitia mabao ya Timonah Wanyonyi, Eli Asieche na Brian Nyakan (mawili) mjini Narok.
Ushindi huo uliwezesha Sofapaka kuruka juu kutoka 13 hadi nafasi ya sita kwa alama nne.
Wanabenki wa KCB, ambao waliingia mechi za raundi ya tatu wakishikilia uongozi, wamesukumwa chini hadi nafasi ya saba.
Wamesalia na alama nne baada ya kunyamazishwa na Gor. Wanafuatiwa na Nzoia Sugar, ambao walilipua washiriki wapya Kisumu All Stars 2-0 kupitia mabao ya Collins Wakhungu na Leonard Kasembeli. Wanasukari hawa, ambao sasa wana alama nne, walishikilia nafasi ya 14 kabla ya matokeo ya wikendi.
Ulinzi imeteremka nafasi saba hadi nambari tisa baada ya kusimamishwa na Mathare 2-1.
Wanajeshi hawa pia wana alama nne, sawa na nambari 10 Rangers iliyoshuka nafasi tano, na mabingwa wa zamani AFC Leopards, wanaofuata katika nafasi ya 11 baada ya kupiga Wazito 1-0 kupitia bao la John Makwata na kuruka juu nafasi nne.
Mabingwa mara 11 Tusker wanakamata nafasi ya 12 kwa alama nne baada ya kuchabanga Zoo 2-1 mjini Kericho. Timothy Otieno na Luke Namanda walifunga mabao ya Tusker, ambayo ilitunuku Zoo bao la kufuta machozi kupitia Rogers Aloro.
Zoo na SoNy, ambazo zilishikilia nafasi za saba na nane kabla ya wikendi, zimeshuka hadi 13 na 14, mtawalia. Ziko bega kwa bega kwa alama tatu.
Nafasi tatu zinazofuata zinashikiliwa na Wazito, Sharks, Kisumu. Wazito, ambayo ina alama mbili sawa na Sharks, zilishuka nafasi nne nayo Kisumu imeteremka nafasi moja kwa alama moja.
Chemelil inasalia mkiani bila alama.