Michezo

Klabu za EPL zilivyotumia Sh173 bilioni kujisuka upya msimu huu wa 2020-21

October 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na CHRIS ADUNGO

VIKOSI vya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) vilimwaga sokoni kima cha Sh173 bilioni ili kufanikisha uhamisho wa wachezaji mbalimbali kwa minajili ya kampeni za muhula huu wa 2020-21.

Ingawa kiasi hicho kilipungua kwa Sh22.4 bilioni kutoka kwa fedha zilizotumiwa na klabu za EPL msimu uliopita wa 2019-20, matumizi hayo yaliashiria nyongeza ya Sh9.8 bilioni kwa kiwango kilichotumika mnamo 2016.

Chelsea ndio walioongoza orodha ya klabu zilizojishughulisha zaidi katika soko la uhamisho muhula huu baada ya kufungulia mifereji yao ya fedha na kumwaga sokoni kima cha Sh31.6 bilioni.

Mabingwa hao wa 2016-17 walijinasia maarifa ya kiungo mvamizi Timo Werner (Sh6.3 bilioni), fowadi Hakim Ziyech (Sh5.2 bilioni), kipa Edourd Mendy (Sh3 bilioni) na Beki Ben Chilwell (Sh7 bilioni).

Kai Havertz ambaye ni sajili ghali zaidi kambini mwa Chelsea msimu huu, aligharimu miamba hao wa soka ya Uingereza kima cha Sh9.8 bilioni kutoka Bayer Leverkusen, Ujerumani.

Chelsea walipata fursa ya kujisuka upya baada ya kupigwa marufuku ya kusajili wachezaji wapya msimu uliopita walipokiuka kanuni za matumizi ya fedha kwa mujibu wa sheria za Shirikisho la Soka la bara Ulaya (Uefa). Isitoshe, kikosi hicho cha kocha Frank Lampard kilipata kiasi kizuri cha fedha baada ya kuwauza Alvaro Morata na Mario Pasalic.

Manchester City ndicho kikosi cha pili kilichotumia kiasi kikubwa zaidi cha fedha baada ya kumsajili beki Nathan Ake na kiungo Ferran Torres kwa kima cha Sh5.7 bilioni na Sh5.1 bilioni mtawalia.

Baada ya kupokezwa kichapo cha 5-2 kutoka kwa Leicester City mnamo Septemba 27, 2020, kocha Pep Guardiola alijibu kipigo hicho kwa kumsajili beki matata raia wa Ureno, Ruben Dias ambaye aliagana na Benfica kwa Sh9 bilioni.

Licha ya Sh14 bilioni walizozitumia katika msimu wa 2019-20 kutowavunia matunda bora, Aston Villa walijishughulisha tena msimu huu kwa kutumia Sh11 bilioni kujinasia huduma za wanasoka watano wakiwemo kiungo Ross Barkley, wing’a Bertrand Traore, mfumaji Ollie Watkins, kipa Emiliano Martinez na beki Matty Cash.

Limbukeni Leeds United nao hawakuachwa nyuma kadri wanavyojizatiti kutia fora kwenye kivumbi cha EPL wanachorejea kukinogesha baada ya miaka 16. Kikosi hicho cha kocha Marcelo Bielsa kiliweka mezani kima cha Sh11.8 bilioni kusajili wanasoka Moreno Rodrigo, Robin Koch, Diego Llorente na Raphinha Dias Belloli.

Wolves waliongeza idadi ya wanasoka raia wa Ureno kambini mwao kwa kutumia Sh9.8 bilioni kutoka jumla ya Sh11.7 kujinasia maarifa ya Fabio Silva na Nelson Semedo. Kikosi hicho cha kocha Nuno Espirito kilisajili pia wachezaji Fernando Marcal na Ki-Jana Hoever kutoka Lyon na Liverpool mtawalia.

Mgongo wa Wolves ulifuatwa kwa karibu na mabingwa watetezi wa EPL, Liverpool waliomwaga sokoni kima cha Sh11.4 bilioni kusajili fowadi Diogo Jota (Sh6.3 bilioni) na kiungo Thiago Alcantara (Sh3.7 bilioni) kutoka Wolves na Bayern Munich mtawalia. Kikosi hicho kinachonolewa na kocha Jurgen Klopp kilisajili pia chipukizi Kostas Tsimikas ili kutoa ushindani kwa beki Andrew Robertson.

Arsenal ndio waliofuata Liverpool baada ya kutumia jumla ya Sh11.4 bilioni kujinasia huduma za beki Gabriel Magalhaes, kipa Runar Alex Runarsson na kiungo matata aliyeagana na Atletico Madrid, Thomas Partey (Sh6.3 bilioni).

Everton walitumia kima cha Sh9.1 bilioni kujinasia huduma za wanasoka Robin Olsen, Ben Godfrey, Allan Marques, Abdoulaye Doucoure, James Rodriguez na Niels Nkounkou.

Kwa upande wao, Tottenham Hotspur walitumia Sh8.7 bilioni kurasimisha uhamisho wa Gareth Bale, Pierre-Emile Hojbjerg, Matt Doherty na Sergio Reguilon.

Manchester United ambao walisajili fowadi Edinson Cavani, Alex Telles na chipukizi Amad Diallo na Facundo Pellistri katika siku ya mwisho ya uhamisho walitumia kima cha Sh7.6 bilioni kujisuka upya. Kikosi hicho cha kocha Ole Gunnar Solskjaer kilijinasia pia maarifa ya kiungo Donny van de Beek kutoka Ajax ya Uholanzi.

Fedha zilizotumiwa na Man-United zilipungua kwa Sh196 milioni pekee kufikia kiasi kilichomwagwa sokoni na Sheffield United waliosajili kipa Aaron Ramsdale wa Bournemouth na fowadi Rhian Brewster kutoka Liverpool.

Sajili mkuu wa Leicester City alikuwa Timothy Castagne ambaye kocha Brendan Rodgers atapania kumfanya kizibo cha Chilwell aliyetua Chelsea. Leicester walitumia jumla ya Sh7.2 bilioni huku Newcastle United wakiweka mezani kima cha Sh4.9 bilioni kwa minajili ya huduma za wanasoka Callum Wilson na Jamal Lewis.

Southampton walioagana na wachezaji Guido Carrillo, Wesley Hoedt na Sofiane Boufal, walitumia Sh4.9 bilioni kujitwalia maarifa ya Kyle Walker-Peters, Mohammed Salisu na Ibrahima Diallo.

Limbukeni West Brom na Fulham walitumia Sh3.8 bilioni na Sh3.2 bilioni mtawalia huku Crystal Palace wakiweka mezani Sh2.8 bilioni kuwasajili chipukizi Eberechi Eze na Nathan Ferguson.

Kiasi hicho cha fedha ndicho kilichotumiwa pia na West Ham United walioagana na kiungo wa zamani wa Arsenal, Jack Wilshere kumsajili Tomas Soucek na Vladimiri Coufal.

Brighton walitumia Sh1.8 bilioni kujitwalia huku Burnley waliojinasia maarifa ya Dale Stephens na Will Norris wakikosa kuweka mezani kiasi chochote cha fedha.

KLABU                          KIASI CHA FEDHA

Chelsea                          Sh31.6 bilioni

Man-City                       Sh20.5 bilioni

Aston Villa                    Sh11.9 bilioni

Leeds United                Sh11.8 bilioni

Wolves                           Sh11.7 bilioni

Liverpool                       Sh11.4 bilioni

Arsenal                           Sh11.4 bilioni

Everton                          Sh9.1 bilioni

Tottenham                    Sh8.8 bilioni

Man-United                  Sh7.6 bilioni

Sheffield Utd                 Sh7.4 bilioni

Leicester City                Sh7.2 bilioni

Newcastle Utd              Sh4.9 bilioni

Southampton                Sh4.8 bilioni

West Brom                     Sh3.8 bilioni

Fulham                           Sh3.2 bilioni

Crystal Palace                Sh2.8 bilioni

West Ham Utd              Sh2.8 bilioni

Brighton                         Sh1.8 bilioni

Burnley                           Sh0