Klabu za Kenya katika hatari ya kutemwa kwenye michuano ya CAF iwapo Ligi Kuu ya FKFPL haitarejelewa kufikia Novemba
Na CHRIS ADUNGO
AFISA Mkuu Mtendaji wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Barry Otieno ameonya kwamba klabu za humu nchini huenda zikajipata katika hatari ya kutonogesha vipute cha kimataifa barani Afrika msimu ujao iwpao kampeni za Ligi Kuu ya Kenya haitaanza kufikia Novemba.
FKF tayari imetoa ratiba ya mechi za Ligi Kuu ya FKFPL kwa minajili ya muhula ujao wa 2020-21 ambapo mabingwa watetezi na washindi mara 19, Gor Mahia watashuka dimbani kuvaana na wafalme mara 11 Tusker FC mnamo Novemba 21.
Mechi hiyo itapigwa siku moja baada ya AFC Leopards, ambao wamenyanyua taji la Ligi Kuu mara 13, kufungua msimu kwa kuwaalika Western Stima mnamo Novemba 20.
Hata hivyo, kuanza kwa kampeni za ligi hiyo ya vikosi 18 kunategemea ufanisi wa FKF kupata idhini ya serikali ambayo imeorodhesha soka miongoni mwa michezo ya kugusana na iliyo hatari zaidi katika kuchangia maambukizi ya virusi vya corona.
Soka ni miongoni mwa michezo ambayo Wizara ya Michezo iliondoa kwenye orodha ya fani kadhaa ambazo ziliidhinishwa kurejelea mazoezi na mashindano ya kawaida mnamo Septemba 18.
“Iwapo hatutaanza ligi kufikia katikati ya Novemba, basi klabu za Kenya zitakuwa katika hatari ya kutemwa kwenye vibarua vya kimataifa. Pigo zaidi huenda ni marufuku ya muda mrefu kwenye vipute vya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) iwapo ligi yetu haitakamilika katika kipindi kinachowiana na kalenda ya CAF,” akasema Otieno.
“Ingawa hivyo, tunashiriki mazungumzo na Wizara ya Michezo na wadau wengine katika serikali kwa kuzingatia hali tete iliyozuliwa na janga la corona. Matarajio yetu ni kwamba tutakubaliwa kurejea ugani chini ya masharti makali yanayodhibiti msambao wa Covid-19,” akaelezea kinara huyo.
Kwa mujibu wa Otieno, ni muhimu sana kwa Ligi Kuu kurejelewa kwa sababu wanasoka wengi wa timu ya taifa ya Harambee Stars ambayo kwa sasa ina kibarua cha kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2021 ni wachezaji wa vikosi mbalimbali vya FKFPL.
Stars wameratibiwa kupepetana na Comoros jijini Nairobi mnamo Novemba 11 kabla ya kurudiana siku nne baadaye jijini Moroni katika mechi mbili zijazo za Kundi G kufuzu kwa fainali za AFCON 2021 nchini Cameroon. Kundi hilo linajumuisha pia Togo na mabingwa mara saba, Misri.
Stars walianza kampeni zao za kufuzu kwa fainali zijazo za AFCON dhidi ya Misri kwa sare ya 1-1 mnamo Novemba 14, 2019 ugenini kabla ya kusajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Togo mnamo Novemba 18, 2019 jijini Nairobi.
Miongoni mwa masharti ambayo FKF imekiri kwamba itawawia vigumu kutekeleza baada ya kurejelewa kwa soka ya humu nchini ni jinsi ya kuzuia mashabiki kuingia katika baadhi ya viwanja visivyo na nyua, malango yatakayohakikisha kuwepo kwa utaratibu wa wachezaji, maafisa wa mechi, mashabiki na wadau wengine kuingia na kutoka uwanjani.
“Itakuwa rahisi mno kudhibiti mashabiki katika viwanja vya Nyayo, MISC Kasarani na Narok. Lakini haiwezekani kwa mechi zote kusakatiwa katika viwanja hivyo,” akasema Otieno.