Klabu za soka ya Ligi Kuu Kenya zachangamkia dili kati ya FKF na BetKing
Na CHRIS ADUNGO
KLABU zinazoshiriki Ligi Kuu ya Kenya zimechangamkia dili ya udhamini kati ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) na kampuni ya mchezo wa kamari ya BetKing.
Betking ni kampuni ya kamari yenye mizizi yake nchini Nigeria.
Udhamini huo wa Sh1.2 bilioni utaanza kutekelezwa rasmi mnamo Septemba 2020 na utadumu kwa kipindi cha miaka mitano ijayo huku kila kikosi kati ya 18 vya Ligi Kuu ya Kenya kikitia kapuni Sh8 milioni kwa mwaka.
Nick Mwendwa ambaye ni Rais wa FKF pia ametangaza kuwa mkataba wa KPL ambayo ni kampuni iliyokuwa ikiendesha Ligi Kuu ya humu nchini hautarefushwa baada ya kutamatika rasmi mnamo Septemba na kwa sasa kuna mjadala wa kuteua jina la Ligi Kuu ya Kenya ambayo huenda ikaitwa FKFPL, BPL au BKPL.
Mwendwa anatazamia msimu ujao wa 2020-21 katika soka ya Kenya kuanza Oktoba 2020 na FKF kwa sasa inajitahidi kutafuta kampuni au bodi itakayoidhinishwa na vikosi vya Ligi Kuu kuendesha kivumbi hicho. Makao makuu ya Bodi ya Usimamizi ya waendeshaji wapya wa Ligi Kuu yatakuwa katika uwanja wa Kasarani.
Kwa mujibu wa John Tonui ambaye ni mwenyekiti wa Posta Rangers, udhamini mwa Betking utaimarisha na kuboresha zaidi viwango vya ushindani miongoni mwa washiriki wa Ligi Kuu ya humu nchini.
“Ingawa tumekuwa tukilipa mishahara ya wachezaji wetu hapo awali, udhamini huu utatuwezesha kuanza kuwapa wanasoka marupurupu na bonasi. Hatua hii itainua maisha ya wachezaji, makocha, marefa na wadau wote wengine wa Ligi Kuu ya Kenya. Wachezaji watahamasika zaidi na hivyo kuimarisha viwango vya ushindani,” akasema Tonui.
Kauli ya Tonui ilipigiwa chapuo na mwenyekiti wa Western Stima, Laban Jobita ambaye alisisitiza kuwa ufadhili wa Betking utawasaidia sana hasa ikizingatiwa kwamba waliokuwa wadhamini wao, kampuni ya umeme ya Kenya Power & Lighting walikatiza ufadhili wao kuanzia Juni 2020.
“Sh8 milioni kwa msimu mmoja ni bora kuliko mifuko mitupu. Msimu uliopita wa 2019-20 ulikuwa mgumu zaidi kwa washiriki wote wa Ligi Kuu huku uchechefu wa fedha ukichangia kuondolewa kwa SoNy Sugar mapema baada ya kushindwa kunogesha mechi tatu za ligi,” akasema mwanasoka huyo wa zamani wa Gor Mahia katika kauli iliyoungwa na mwenyekiti wa Kariobangi Sharks, Robert Maoga ambaye pia alisisitiza kuwa udhamini wa Betking utarejesha hadhi ya soka ya Kenya.
Hata hivyo, Cleophas Shimanyula ambaye ni mwenyekiti wa Kakamega Homeboyz amemkosoa Mwendwa kwa kutoshauriana na klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Kenya kabla ya kuanza na hatimaye kurasimisha dili kati ya FKF na Betking.
Shimanyula pia ametilia shaka uhalali wa dili hiyo hasa ikizingatiwa kwamba hakuna mwakilishi yeyote wa Betking aliyekuwepo wakati Mwendwa alipozindua rasmi ufadhili huo wa Sh1.2 bilioni mnamo Julai 16, 2020 katika jengo la Kandanda House, Nairobi.