Klopp aponyokwa na Timo Werner, atua Chelsea
Na CHRIS ADUNGO
CHELSEA wameafikiana na RB Leipzig kuhusu usajili wa fowadi Timo Werner ambaye anatarajiwa kutua ugani Stamford Bridge mwishoni mwa msimu huu.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 ambaye amepachika wavuni jumla ya mabao 25 katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) hadi kufikia sasa atawagharimu Chelsea kima cha Sh7.5 bilioni.
Awali, Werner alikuwa akihusishwa na uwezekano mkubwa wa kuingia katika sajili rasmi ya Liverpool na akasema “itakuwa tija na fahari kubwa sana” kuvalia jezi za miamba hao wa soka ya Uingereza chini ya kocha mzawa wa Ujerumani, Jurgen Klopp.
Hata hivyo, Liverpool kwa sasa wameshikilia kwamba hawazihitaji huduma za Werner ambaye ameifungia timu ya taifa ya Ujerumani jumla ya mabao 11 kutokana na mechi 29 zilizopita.
Mwezi jana, mshambuliaji mzawa wa Ufaransa, Olivier Giroud alirefusha mkataba wake kambini mwa Chelsea kwa kipindi cha mwaka mmoja zaidi. Uwepo wake utachangia utajiri wa tajriba itakayowatambisha chipukizi Tammy Abraham na Christian Pulisic wanaotazamiwa kushirikiana vilivyo na Werner.
Werner anakuwa sajili wa pili wa Chelsea kwa minajili ya kampeni za msimu ujao. Mnamo Februari 2020, kikosi hicho cha kocha Frank Lampard kilimsajili winga Hakim Ziyech aliyehiari kuagana na Ajax Amsterdam ya Uholanzi kwa kima cha Sh5.2 bilioni.
Werner amekuwa tegemeo kubwa la Leipzig tangu asajiliwe na kikosi hicho kutoka Stuttgart mnamo 2016.
Alipachika wavuni jumla ya mabao matatu katika ushindi wa 5-0 uliosajiliwa na Leipzig dhidi ya Mainz mnamo Mei 24, 2020. Alifunga magoli matatu mengine katika ushindi mnono wa 8-0 waliousajili dhidi ya Mainz kwenye mchuano wa mkondo wa kwanza wa Bundesliga mwishoni mwa mwaka uliopita.
Mnamo Januari 2020, kocha Lampard alikuwa akihusishwa na fowadi mkongwe wa Paris Saint-Germain (PSG), Edinson Cavani pamoja na mfumaji matata wa Napoli, Dries Mertens. Hakuna yeyote kati ya hao ambaye alifaulu kusajiliwa na Chelsea.