• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
KNH sasa yajitahidi kuaga Ligi ya Daraja la Pili

KNH sasa yajitahidi kuaga Ligi ya Daraja la Pili

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) inazidi kupiga hesabu zake maana inaendelea kupitia pandashuka sio haba michezoni.

KNH ya kocha, George Makambi ni kati ya timu 38 zinazoshiriki kampeni za Ligi ya Taifa Daraja la Pili msimu huu.

Kocha huyo anasema ”Miaka yote huanza ligi kwa kusudio moja kupanda ngazi kushiriki Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza lakini mpango wetu huenda mrama tukikaribia kukamilisha mechi za mkumbo wa pili,” alisema na kuongeza kuwa uhaba wa ufadhili umeibuka donda sugu kwa kikosi hicho. Alisema kwa kikosi chochote kufanya vizuri katika soka kinahitaji mtaji mrefu ili kusaka sajili za wanasoka wazuri.

Anadokeza kwamba kwenye mechi za ngarambe ya msimu huu vijana wake wamo kati ya nafasi tano bora wanakolenga kujituma kiume kukabili wapinzani wao kupigania kuibuka kidedea.

Licha ya kushuka na kupanda kwenye michezo ya Kundi A, KNH inaorodheshwa kati ya vikosi vinavyotesa siyo haba msimu huu. Aidha kocha huyo anafunguka kuwa anatamani sana kuona KNH inasonga mbele kushiriki Ligi za upeo wa juu nchini.

Pia alidai hakuna mwanadamu hasiyependa maendeleo ndiyo maana wangali mbioni kwenye jitihada za kutafuta tiketi ya kusonga mbele. Makambi anasema anatamani sana kufuata timu waliowahi shiriki ligi moja ikiwamo Bidco United, Bandari FC, Sofapaka FC kati ya zingine.

”KNH imeshiriki Ligi ya Taifa kwa muda mrefu na bila shaka wachana nyavu wangu watafurahi sana endapo watafaulu kunasa tiketi ya kupandishwa ngazi,” alisema. Kocha huyo anakiri kwamba kampeni za msimu zimeshuhudia upinzani wa nguvu kinyume na matarajio ya wengi.

Wachezaji wa KNH wakipasha misuli moto. Picha/ John Kimwere

Kwenye jedwali, KNH inashikilia nafasi ya tatu kwa alama 33, mbili mbele ya Mwiki United. Uweza FC ya kocha, Charles ‘Stam’ Kaindi inaongoza kipute hicho kwa alama 38, moja mbele ya Balaji EPZ.

Ili kukamilisha ratiba ya msimu huu imepangwa kukabili Jumbo T pia Kenafric vikosi anavyosema kwamba kamwe havieleweki. Kadhalika kikosi hicho kitakamilisha shughuli nzima kitakapoingia mjegoni kucheza na Zetech University.

“Soka limejaa changamoto nyingi tu ikiwamo kugharamia mahitaji muhimu ili kufanikisha shughuli nzima, lakini lina faida kubwa hasa kwa timu zinazoshiriki ligi za viwango vya juu nchini,” alisema.

Soka ni ajira kama nyingine maana inalipa pesa ndefu kwa wachezaji walioiva vizuri na kuhitimu kushiriki mechi za kimataifa. KNH inajivunia kulea wachezaji wengi tu waliowahi kuteuliwa kuchezea klabu mbali mbali nchini bila kuweka katika kaburi la sahau Harambee Stars.

Miongoni mwao wakiwa Nicholas Muyoti aliyegeukia ukufunzi. Pia amewahi chezea AFC Leopards na Thika United kati ya klabu zingine.

Imewahi noa makucha zake Danson Kago, awali akichezea Sofapaka FC, Mike Obonyo aliyekuwa akipigia Re-union kabla ya kustaafu.

Wengine wakiwa Mulinge Ndeto, Joseph Njuguna aliyewahi kuchezea Gor Mahia FC, Anthony Muki Kimani awali alibahatika kusakatia Sofapaka FC na Kevin Ouma aliyewahi kuchezea Mathare United.

Anashukuru wasimamizi wa Hospitali ya Kenyatta ambao wameonyesha moyo wa kukuza talanta za soka na kuendelea kushikilia timu hiyo kuendeleza shughuli zake michezoni. Anatoa mwisho kwa wahisani wajitokeze kuzipiga jeki klabu za mashinani ambazo zimejitwika jukumu la kulea wachezaji chipukizi.

KHN inajumuisha wachezaji kama: Isaac Njoroge, Jackson Obuchere, Michael Opunde, Ben Obiri, Mkaa Chacha, Brian Otieno, Nigel Wijira, Timothy Wekesa na Ange Fabrice. Pia wapo Alla Laurent, Isiake Ajenje, Selestine Dimarere, Mbaga John, Makomere Victor, Fabian Otieno, Ivans Miiro na Kibugi Samuel.

You can share this post!

Hospitali zisizotibu wanafunzi kuona cha moto

Kalonzo ataka wanaobwagwa kwa urais wapewe ubunge

adminleo