• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:55 AM
Kocha Baraza ala mori Sofapaka itazima Gor leo Jumatano

Kocha Baraza ala mori Sofapaka itazima Gor leo Jumatano

Na CECIL ODONGO

MABINGWA wa Ligi Kuu (KPL) 2010 Sofapaka, wameapa kuzima Gor Mahia, timu hizo zitakapokabiliana leo Jumatano kwenye mechi ya ligi itakayogaragazwa ugani Moi, jijini Kisumu.

Katika mechi nyingine, Zoo Kericho watakuwa wenyeji wa mabingwa wa 2008 Mathare United mjini Kericho.

Kocha wa Sofapaka, John Baraza alieleza ‘Taifa Leo’ kwamba vijana wake wako na ari ya kutwaa ushindi huo, kwa kupokeza K’Ogalo kichapo cha tatu tangu msimu huu uanze.

Gor wamepoteza dhidi ya Mathare United na Kakamega Homeboyz pekee msimu huu.

Licha ya kutoka sare ya 1-1 na wavuta mkia Chemelil wikendi iliyopita, Baraza ana imani kwamba wanahitaji ushindi kivyovyote vile hii leo ili kuhakikisha wanatoa ushindani kwa timu zilizo nafasi za juu ligini.

“Tunaelekea Kisumu tukiwa na nia ya kutifua vumbi na kuwa timu ya tatu kulaza Gor Mahia kwenye KPL msimu huu. Vijana wangu wana ari ya kucheza kwa kujituma ili kuhakikisha kwamba tunaibuka na ushindi,” akasema Baraza.

“Japo tulilazimishwa sare ya 1-1 na Chemelil, wanaotukosoa kwa kucheza vibaya wanafaa kufahamu kwamba hakuna timu ndogo au kubwa uwanjani. Sare hiyo imetupa motisha zaidi kwamba hata sisi tunaweza tukawaangusha miamba Gor Mahia kwao,” akaongeza.

Sare itaiwezesha K’Ogalo kupanda hadi kileleni mwa msimamo wa jedwali la Ligi Kuu(KPL) huku ushindi kwa Sofapaka ukiwapaisha hadi nafasi ya sita ligini.

Katika mechi ya pili, mkufunzi wa Mathare United Salim Ali naye ameahidi kulipua Zoo FC, timu hizo zikigaragazana mjini Kericho. Ali ambaye alikiri kwamba vijana wake wamekuwa wakipata matokeo mabaya, alitaja mechi ya leo kama mwanzo wa mwamko mpya kambini mwa mabingwa hao wa zamani.

“Tumekuwa na tatizo hasa katika safu yetu ya ushambulizi lakini tumepumzika vya kutosha na tunalenga ushindi leo ili kupata motisha ya kung’aa kwenye mechi zajazo,”

“Wachezaji wangu wazoefu walihamia timu nyingine na kwa sasa tunapitia muda wa mpito kwa kuwatumia wachezaji chipukizi na wengine tuliowanunua. Mbinu zao za mchezo bado hajizaoana ndiyo maana tumekuwa tukitatizika sana mchezoni,” akasema Ali.

Ushindi kwa Zoo utawapaisha hadi nafasi ya 11 mbele ya Bandari huku Mathare wakiomba Sofapaka icharazwe nao washinde ili wapae hadi nafasi ya tisa.

You can share this post!

WAKO NDANI: Arsenal kifua mbele FA

Rais amkemea vikali mbunge

adminleo