Michezo

Kocha David Maina asema malkia wa vikapu Equity Bank Hawks kuendelea kutawala ligi ya nyumbani

May 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 4

Na GEOFFREY ANENE

MALKIA wa Ligi Kuu ya mpira wa vikapu nchini, Equity Bank Hawks wana matumaini makubwa watazidi kutesa nyumbani baada ya janga la virusi vya corona kudhibitiwa.

Vipusa hao wa kocha David Maina, ambao walipepeta miamba Halmashauri ya Bandari za Kenya (KPA) katika fainali ya ligi mwaka 2018 na 2019, pia wameapa kunyakua taji la Afrika Mashariki na Kati, ambalo walipoteza mwaka 2019.

Wanabenki hao walikuwa wamefanya mazoezi majuma matatu kabla ya serikali kupiga marufuku mikusanyiko mwezi Machi ili kuzuia maambukizi ya virusi hivyo. Equity Hawks pia ilikuwa imeandaa majaribio ya kutafuta wachezaji wa kuimarisha kikosi chake.

Majaribio hayo yalikuwa wazi kwa wanafunzi waliopata alama nzuri, ambao wanaweza kuajiriwa na benki hiyo. Yalivutia zaidi ya wanafunzi 30 kutoka vyuo vikuu vya USIU, Kenyatta, Mount Kenya na Co-operative, miongoni mwa vingine.

Maina aliambia Taifa Leo kuwa janga la virusi vya corona halijawazuia kufanya mazoezi wala kuwazia jinsi ya watakavyopata mafanikio zaidi. “Tumekuwa tukitumia wachezaji video na mafunzo muhimu ambayo wanafaa kuyafuata kwa makini nyumbani pekee yao. Baada ya kupitia mafunzo hayo na video, wanaturudishia ili tuweze kuthibitisha kuwa wanatimiza malengo ya timu,” alisema Maina katika mahojiano jijini Nairobi.

“Tunalenga kutetea ubingwa wetu wa kitaifa msimu huu. Tunatumai tutakuwa na mtazamo mzuri, mtazamo ambao tulikuwa nao wakati wa mechi za muondoano za kukamilisha msimu 2019 wakati tulijituma kujaza pengo la nyota wetu Betty (Kananu). Aliumia mguu na kukosa mechi za muondoano. Tulikubaliana kuwa lazima tujaze mwanya ulioachwa na Betty. Mchezaji Annrose Atieno alikuwa kizibo tosha cha Betty, na hiyo ndiyo sababu tulipata matokeo mazuri.”

Kananu tayari ameanza mazoezi mepesi ya kukimbia, ingawa Maina anaamini huenda asichangie pakubwa katika mkondo wa kwanza wa ligi.

“Huenda hatutamtegemea msimu ukianza. Tutampatia muda wa kutosha awe sawa kimwili na kupona kabisa. Tunataka kuanza kumwazia Betty tutakapoingia mechi za ligi za mkondo wa pili. Anaweza kufanya nasi mazoezi katika mkondo wa kwanza, lakini hatutaki kumharakisha ama kufanya awe na presha,” alisema.

Sababu ya Equity kuanza mikakati ya kuunda timu mpya, Maina alisema, ni kuhakikisha ina wachezaji wa kutosha kushiriki kwenye ligi pamoja na mashindano mengine yakiwemo mashindano ya benki. “Kama benchi ya kiufundi, tunataka kupata wachezaji ambao wanaweza kuchukua nafasi ya wachezaji ambao wanaelekea kustaafu,” aliongeza kocha huyo.

“Tulitambua wachezaji wanne ama watano wakati wa majaribio, ambao umri wao bado ni mdogo. Naamini tukiwapa fursa, watajaza vyema nafasi za wachezaji wazee, ambao wako kikosini.” Wachezaji wapya ambao tayari majina yao yanajulikana ni Maryann Nyagaki na Jemimmah Night.

Kwa mujibu wa Maina, wachezaji hao wapya wako tayari kujiunga na timu ya Equity mara tu ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona utakapodhibitiwa. “Tutawapatia fursa ya kuonyesha talanta yao uwanjani. Tutakuwa na timu mbili – moja ya wachezaji wazuri kabisa na timu ya pili ya wachezaji wanaoweza kuingia timu ya kwanza. Yeyote atakayelegea katika timu ya kwanza ama kuumia atashushwa katika timu ya pili na nafasi yake kutwaliwa na mchezaji mzuri kutoka timu ya pili. Tumeamua kuwa na timu mbili ilikuwekea kila mchezaji presha ya kujituma zaidi.”

Aidha, Maina amelalamikia Kenya kukosa wachezaji warefu. “Tuko na wachezaji wafupi. Hii imeathiri timu zetu nyingi.”

Kuwa mabingwa, anasema Maina, ni kitu kizuri.

“Kila timu sasa inakazana kutafuta mbinu ya kutupiga. Kusema kweli, sisi bado ni ‘moto wa kuotea mbali’ kuliko wapinzani wetu ligini msimu huu. Inahuzunisha kuwa bado naona fainali ya ligi ya msimu huu ikiwa kati ya Equity na timu ya KPA. Hi ni kwa sababu idadi ya timu zenye ushindani ni chache. Huwa tunapata timu kama sita hivi zilizo na ushindani, lakini mechi zetu nyingi huwa ni mswaki. Hii hutuathiri sana katika mechi za kimataifa kwa sababu kule hakuna mchezo; mechi zote ni moto. Sisi kama Equity, tunalenga kudumisha matokeo yetu mazuri. Tunalenga kuhifadhi taji letu na kurejea katika mashindano ya Afrika Mashariki na Kati, na kunyakua taji tulilopoteza. Tunataka pia kuimarisha matokeo yetu kwenye mashindano ya Bara Afrika. Tulifanya vibaya sana tuliposhiriki mashindano ya Afrika, lakini naamini tukipata tiketi tena, hatutaenda huko kuwa watalii, bali washindani.”

Kuhusu jinsi Hawks imekuwa ikichangia katika vita dhidi ya janga la corona, Maina alisema, “Bado tunafanya mipango ya kusaidia walioathirika na ugonjwa wa Covid-19. Hata hivyo, sisi kama timu pia tumekuwa tukihamasisha wachezaji wetu kuhusu umuhimu wa kutokaribiana, kunawa mikono na kujiweka salama. Janga hili limeathiri dunia nzima na inafaa tujifunze jinsi ya kuishi tukifahamu lipo. Maisha yetu lazima yaendelee baada ya janga hili.”

Kuhusu siri ya Equity kupata mafanikio, Maina alisema kuwa wamepatia nidhamu kipaaumbele. “Tumekuwa mabingwa mara tatu wa Kenya. Tulishinda ligi mwaka 2015 halafu tena 2018 na 2019. Pia, tulinyakua taji la Afrika Mashariki na Kati nchini Tanzania mwaka 2018. Siri ya mafanikio haya ni nidhamu yetu kama timu na pia kufahamu tunawakilisha kampuni kubwa ya Equity,” alisema.

Kwa kipindi cha miaka saba, ambayo klabu ya Equity imekuwa, Maina anasema kuwa hajawahi kusumbuana na wachezaji. “Sijasikia kitu ambacho kimenifanya nihisi hatuhitaji mchezaji huyu ama yule kwenye timu kwa sababu ya suala la nidhamu. Tumewapatia sheria na wamekuwa wakizifuata bila ya kuzikiuka,” alisema kocha huyo.

Maina pia alizungumzia maisha yake akiwa Equity. “Kabla nije Equity miaka saba iliyopita, nilikuwa nimefundisha timu za wanaume pekee tangu mwaka 1997. Ilikuwa changamoto kubwa kuanza kuongoza timu ya wanawake ya Equity, lakini sijutii hatua hii niliyochukua. Nakiri kuwa miaka miwili ya kwanza ilikuwa balaa kubwa. Kufanya kazi na wanawake na ulikuwa umezoea kufanya kazi na wanaume si kazi rahisi. Lazima uwaelewe. Hata hivyo, kwa neema na Mungu, nimefanikiwa kufanya haya yote. Siwezi kupuuza benchi ya kiufundi, nahodha, wachezaji wengine na uongozi wa benki ya Equity kwa jumla. Wote wamechangia katika mafanikio haya,” alisema Maina.

Alidokeza kuwa sababu kuu iliyochangia Equity kupoteza ubingwa wa Afrka Mashariki na Kati mwaka 2019 ni kujeruhiwa kwa tegemeo Kananu.

“Mwaka 2019 tulirudi Tanzania tulikokuwa tumeshinda taji la Afrika Mashariki na Kati mwaka 2018. Tulikuwa na matarajio makubwa kuwa tutatetea ubingwa wetu. Hata hivyo, wakati mwingine unaweza kujiandaa vizuri, lakini unapofika mashindanoni mambo hayaendi jinsi ulivyopanga. Nakumbuka mechi iliyozima ndoto yetu ilikuwa dhidi ya timu ya JKL Dolphins kutoka Uganda wakati Kananu alijeruhiwa kisigino. Ilikuwa pigo kubwa kwetu kwa sababu motisha ya wachezaji wengine ilishuka. Kutoka hapo, wahakuwa na moyo wa kupigania ushindi. Badala ya kubadilisha mtazamo wetu na kujitolea kushinda mchuano huo kama njia ya kumpatia zawadi Betty, wachezaji walilaza damu na tukapoteza mchuano huo na pia mechi iliyofuata. Nadhani, tulipoteza taji kwa sababu tulipoteza Betty. Yeye hutoa mchango mkubwa katika timu ya Equity. Amekuwa mchezaji wa kutegemewa katika mechi zetu nyingi. Ameibuka mfungaji bora wa Equity mara nyingi katika msimu wa kawaida pamoja na katika mechi za kumalizia msimu. Anafahamu jinsi ya kuwatia msukumo wachezaji wenza na ametusaidia sana katika kupata matokeo mazuri.”

Ligi ya mpira wa vikapu ya Kenya ilitarajiwa kuanza Machi kabla ya serikali kupiga marufuku mikusanyiko ya watu ili kuzuia maambukizi ya virusi vya corona, ambavyo vimeua watu 50 humu nchini. Watu 1,161 wamethibitishwa kuwa na virusi hivyo Kenya.