Michezo

Kocha Joachim Loew aponea shoka katika timu ya taifa ya Ujerumani

December 1st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

KOCHA wa timu ya taifa ya Ujerumani, Joachim Loew ataendelea kudhibiti mikoba ya kikosi hicho na atasimamia kampeni zilizoahirishwa za Euro 2021 licha ya mabingwa hao wa zamani wa dunia kusajili msururu wa matokeo dunia chake yake.

Kudumishwa kwa Loew kambini mwa Ujerumani kumethibitishwa na Shirikisho la Soka la Taifa hilo (DFB) ambalo liliandaa mkutano wa dharura mnamo Novemba 30, 2020 ili kutathmini matokeo ya kikosi na kuweka mpango mkakati wa kunyanyua miamba hao wa soka duniani.

“Kamati Kuu ya DFB imeamua kwa kauli moja wakati wa mkutano wa mtandaoni ulioandaliwa Novemba 30, kwamba Joachim Loew ataendelea kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa licha ya kudidimia kwa ubora wa matokeo ya kikosi tangu Machi 2019,” ikasema sehemu ya taarifa hiyo.

Loew, 60, amekuwa mkufunzi wa Ujerumani tangu 2006 alipoaminiwa kuwa mrithi wa Jurgen Klinsmann aliyepokonywa mikoba ya kikosi mwishoni mwa fainali za Kombe la Dunia.

Chini ya Loew, Ujerumani walitawazwa mabingwa wa Kombe la Dunia mnamo 2014 nchini Brazil. Taji hilo lilikuwa la nne kwa Ujerumani kutia kapuni katika kampeni za kipute hicho.

Ingawa hivyo, Ujerumani wamekuwa wakisuasua katika kipindi cha hivi karibuni huku wakipepetwa 6-0 na Uhispania katika mechi ya UEFA Nations League. Awali, walikuwa wameambulia sare mara mbili dhidi ya Uswisi na Uturuki mara moja.

Kichapo cha 6-0 kutoka kwa Uhispania ndicho kinono zaidi kwa Ujerumani kuwahi kupokea katika kipindi cha miaka 89. Kikosi hicho kimeshuhudia matokeo dunia katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita na kiliondolewa mapema kwenye hatua ya makundi katika fainali za Kombe la Dunia za 2018 nchini Urusi licha ya kuwa mabingwa watetezi.

Tangu wakati huo, Loew amekuwa akifanya maamuzi yenye utata yakiwemo yale ya kutamatisha ghafla taaluma za wanasoka washindi wa Kombe la Dunia – Thomas Mueller, Jerome Boateng na Mats Hummels katika timu ya taifa.