• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Kocha Jurgen Klopp kagombana na hawa wachezaji sita

Kocha Jurgen Klopp kagombana na hawa wachezaji sita

NA LABAAN SHABAAN

KOCHA Jurgen Klopp ni mtu mwenye msimamo thabiti, sifa inayomfanya asiwe mgeni wa kugombana na baadhi ya wachezaji wa timu anazofundisha.

Alisema yeye na mshambuliaji Mohamed Salah–Mo Salah– pale Liverpool wametatua mzozo.

Salah alikuwa kwenye benchi kwenye mechi dhidi ya West Ham United iliyoisha sare ya 2-2.

Klopp aliambia wanahabari kuwa walizika tofuati zao lakini Salah akazua zogo aliposema: “Nikizungumza kutawaka moto.”

Kocha huyu Mjerumani si mgeni kwa mzozo na wachezaji wake. Si kila wanaogombana wanapatana na kufanya kazi pamoja.

Hii ni kwa sababu ya matukio yaliyojiri Klopp akiwa kocha katika klabu za Liverpool na Borussia Dortmund.

Hebu tuwaangazie baadhi ya wachezaji ambao kocha huyu mahiri amekorofishana nao.

Mohamed Salah

Ndiye mchezaji wa hivi punde zaidi katika tukio baya la utengano kati ya wawili ambao wameshinda mataji pamoja.

Klopp alimsalimu kwa mkono Salah aliyetoka kupasha kiti moto na wakaanza kurushiana cheche kabla ya straika Darwin Nunez kuingilia kati.

Dakika chache baadaye Klopp alieleza walizika tofauti zao kwenye kaburi la sahau aliposema.

“Tumeongea nyuma ya pazia na sasa tuko sawa,” akasema Klopp.

Mario Balotelli

Huyu ni straika mbishani ambaye ingeshangaza iwapo asingegombana na Klopp.

Kabla ya Klopp kushika hatamu za uongozi ugani Anfield miaka tisa iliyopita, Balotelli alikuwa tayari keshatua ugani Anfield.

Klopp alimwambia staa huyo wa zamani wa Manchester City na timu ya taifa ya Ujerumani kuwa asingemhusisha katika michuano na hapo mambo yakatibuka.

“Alinieleza kuwa ningekaa lakini singekuwa chaguo lake kwa hivyo akaniambia afadhali niondoke. Lakini nilimwambia kwaheri na hatutaonana tena,” akaripoti Balotelli baada ya kuaga klabu ya Liverpool.

Kwa moto uo huo, wakala wa Balotelli, Mino Raiola, alimkaripia Klopp kwa jinsi alivyomchukulia mchezaji aliyemwakilisha.

Nuri Sahin

Klopp alipokuwa kocha wa Borussia Dortmund nchini Ujerumani, wakati mmoja alimtimua kiungo Nuri Sahin (sasa ni kocha msaidizi Borussia Dortmund) kutoka mazoezini.

“Nafikiri ulikuwa mwaka wa 2009 ama 2010. Nilikuwa ninachezea Borussia Dortmund na kocha akanitimua kutoka mazoezini baada ya kugombana na mchezaji mwingine. Nilikuwa kinda wa soka asiyekuwa na purukushani. Nina uhakika nilikuwa sahihi asilimia 100 lakini aliniambia niondoke, kwa hivyo nikaondoka,” akasema Sahin.

Lazar Markovic

Kama Balotelli, Markovic hakuonekana na umuhimu kwenye kikosi cha Klopp katika klabu ya Liverpool.

Winga huyu alilaumu usimamizi wa Liverpool akisema waliagiza dau kubwa sana wakati wa mauzo yake na kufanya uhamisho wake kuwa mgumu kufanyika.

Alihamishwa kwa mikopo mara nyingi kabla ya kupata uhamisho wa kudumu 2019 alipojiunga na Fulham.

“Waliagiza pesa nyingi sana kufanikisha uhamisho wangu,” alisema Markovic.

“Ni kazi yangu sasa kuonyesha Liverpool kuwa mimi ni yule yule mchezaji na watu wa Liverpool hawafai kunifanyia hivyo.”

Mamadou Sakho

Kiungo huyu alikuwa muhimu sana chini ya aliyekuwa kocha wa Liverpool Brendan Rodgers.

Lakini kitumbua chake na Klopp kiliingia mchanga mwaka wa 2016.

Klopp alisema Sakho alichelewa kuingia mikutanani na kukosa safari ya ndege kwenda Amerika kabla ya kumtimua baadaye akajiunga na Crystal Palace.

“Alichelewa kusafiri nasi kwenye ndege na kukosa mikutano. Ninafaa kuunda kikosi na kwa hivyo niliona afadhali arudi Liverppol,” Klopp alijitetea.

Xherdan Shaqiri

Fowadi huyu Mswizi hakufukuzwa Liverpool na Klopp lakini waliwahi kuzushiana uwanjani kama kisa cha Mo Salah.

Klopp alikimbia ugani kumshambulia Shaqiri baada ya kupoteza mkwaju wa ikabu katika mechi ambayo Liverpool ilibanduliwa kutoka shindano la League Cup 2018.

Mjadala mkali ulijiri ugani kati ya Klopp na Shaqiri na kuvutia maswali kutoka kwa wanahabari.

“Nilizungumza kuhusu mkwaju wa ikabu pekee – ule wa mwisho. Salah alikuwa kando pekee na wachezaji wengine walikuwa wamejikusanya upande mmoja ambapo tulipiga mpira,” Klopp alisema.

“Kama angemmegea Salah katika dakika ya mwisho, matokeo yasingekuwa mabaya. Ilikuwa sababu ya mkwaju huo tu na si mambo mengine,” akaongeza.

  • Tags

You can share this post!

Mabalozi 26 wapya sasa kuanza kazi baada ya kuteuliwa rasmi...

Presha kwa Arsenal ikihitaji pointi 2 kumaliza EPL katika...

T L