Kocha Migne ataja kikosi cha Harambee Stars tayari kwa AFCON
Na GEOFFREY ANENE
SHOKA la kocha mkuu Sebastien Migne limemwangukia Allan Wanga anayeongoza ufungaji wa mabao kwenye Ligi Kuu ya Kenya baada ya kutaja kikosi chake cha Harambee Stars cha wachezaji 27 mnamo Alhamisi kitakachoshiriki Kombe la Afrika (AFCON) nchini Misri mwezi Juni.
Migne na vijana wake, ambao watamenyana na Algeria, Senegal na Tanzania katika mechi za makundi za AFCON, watasafiri nchini Ufaransa hapo Mei 31 kwa kambi ya mazoezi ya wiki tatu.
Mshambuliaji chipukizi wa Sofapaka, John Avire, amepata namba, sawa na wachezaji wazoefu Victor Wanyama, ambaye yuko katika kikosi cha Tottenham Hotspur cha kocha Mauricio Pochettino kitakacholimana na Liverpool katika fainali ya Klabu Bingwa Ulaya hapo Juni 1.
Mfungaji wa mabao mengi ya Stars wakati huu, Michael Olunga, ambaye anasakatia Kashiwa Reysol nchini Japan, pia si sura mpya katika kikosi cha Stars pamoja na winga wa Beijing Renhe Ayub Timbe, ambaye anarejea baada ya kuwa nje kwa muda akitumikia marufuku kwa utovu wa nidhamu na pia majeraha.
Stars itakuwa na kambi ya mazoezi ya siku 19 nchini Ufaransa. Katika kipindi hicho, vijana wa Migne pia watapimana nguvu dhidi ya Madagascar mnamo Juni 7 jijini Paris na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo mnamo Juni 15 jijini Madrid nchini Uhispania.
Itaelekea jijini Cairo nchini Misri mnamo Juni 19. Mechi zake za Kundi C zitakuwa dhidi ya Algeria (Juni 23), Tanzania (Juni 27) na Senegal (Julai 1) uwanjani 30 June Stadium.
Allan Wanga ambaye amefungia Kakamega Homeboyz mabao 18 ameachwa nje.
Atafahamu kama itaibuka mfungaji bora baada ya timu ya Ulinzi Stars kumenyana na Mount Kenya United wikendi hii katika mechi pekee iliyosalia baada ya kuahirishwa kutoka Jumatano. Enosh Ochieng’ amefungia Ulinzi mabao 16.
Kindumbwendumbwe cha AFCON kitakamilika Julai 19.
Kikosi cha Harambee Stars
Makipa
Patrick Matasi, John Oyemba, Faruk Shikalo
Mabeki
Abud Omar, Joash Onyango, Joseph Okumu, Musa Mohammed, David Owino, Bernard Ochieng, Brian Mandela, Philemon Otieno, Eric Ouma
Viungo
Victor Wanyama, Anthony Akumu, Ismael Gonzalez, Ayub Timbe, Francis Kahata, Ovella Ochieng, Dennis Odhiambo, Eric Johanna, Paul Were, Cliffton Miheso, Johanna Omollo
Washambuliaji
John Avire, Masud Juma, Christopher Mbamba, Michael Olunga