Michezo

Kocha Nuno Espirito kurefusha mkataba wake kambini mwa Wolves

September 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

MKUFUNZI Nuno Espirito anatarajiwa kutia saini mkataba mpya kambini mwa Wolves.

Nuno, 46, angali na mwaka mmoja pekee kwenye kanadarasi yake ya sasa na kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Mkufunzi huyo mzawa wa Ureno amekuwa akidhibiti mikoba ya Wolves kwa miaka mitatu iliyopita. Anajivunia kuwaongoza Wolves kupanda ngazi kutoka Ligi ya Daraja la Kwanza (Championship) hadi EPL na kuwachochea kutinga robo-fainali za Europa League kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 50.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uingereza, Nuno amekuwa katika mazungumzo na usimamizi wa Wolves na dalili zinaashiria kuwa atarefusha muda wa kuhudumu kwake ugani Molineux, Uingereza.

“Kuhusu mkataba mpya, sina shaka kuhusu chochote kwa sababu hiyo si kazi. Sina mchango wowote katika kuhakikisha iwapo napokezwa mkataba mpya au la. Langu ni kuwapa wasimamizi msimamo wangu na kusubiri barua-pepe au simu ya kuniambia iwapo matakwa yangu yamekubaliwa,” akasema Nuno.

Wolves wameratibiwa kuanza kampeni za EPL katika msimu mpya wa 2020-21 dhidi ya Sheffield United mnamo Septemba 14, 2020.

Hadi kufikia sasa, kikosi hicho kinachofahamika sana kwa kuwaangusha miamba wa soka ya Uingereza, kinajivunia kusajili wachezaji watatu pekee, akiwemo Fabio Silva, 18, aliyeagana na FC Porto ya Ureno kwa kima cha Sh4.9 bilioni.

Kwa mujibu wa Nuno, matamanio yake ni kusajili wanasoka wawili zaidi akiwemo beki Ainsley Maitland-Niles wa Arsenal ili ajaze pengo lililoachwa na Matt Doherty aliyeyoyomea Tottenham Hotspur.

Arsenal walikuwa wamefichua azma ya kuagana na Maitland-Niles muhula huu kabla ya matokeo mazuri ya Mwingereza huyo katika fainali ya Kombe la FA dhidi ya Chelsea na katika ushindi wa Community Shield dhidi ya Liverpool kumshawishi kocha Mikel Arteta kubadili mawazo ya kumtia mnadani.

Ingawa hivyo, Nuno anaamini kwamba Wolves watawasilisha ofa nzuri kwa Arsenal ili wamwachilie beki huyo wa kulia.