• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 7:55 PM
Kocha wa Bidco United imani tele kikosi chake kitatamba ligini

Kocha wa Bidco United imani tele kikosi chake kitatamba ligini

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Anthony Akhulia wa Bidco United ni mwingi wa imani kwamba sajili wapya kikosini mwake watasajili matokeo ya kuridhisha katika kampeni za msimu ujao wa Ligi Kuu ya Kenya (FKFPL) 2020-21.

Bidco United walinogesha kampeni za Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL) kwa zaidi ya miaka 10 kabla ya kupandishwa daraja kushiriki Ligi Kuu mwishoni mwa msimu uliopita wa 2019-20

Hii ni baada ya kuambulia nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la NSL nyuma ya Nairobi City Stars almaarufu ‘Simba wa Nairobi’.

“Umoja na ushirikiano kikosini ilikuwa siri ya mafanikio yetu msimu uliopita. Sasa tuna kiu ya kuendeleza matokeo hayo bora na tunalenga kujisuka upya ili tuwe na kikosi kitakachotuwezesha kufikia mengi ya malengo yetu,” akasema Akhulia.

Hadi kufikia sasa, Bidco United wamejinasia huduma za wanasoka wapya 11 kwa minajili ya msimu ujao wa 2020-21. Wachezaji 10 kati ya hao wamewahi kushiriki Ligi Kuu ya Kenya. Hao ni pamoja na beki Pistone Mutamba (Wazito FC), fowadi Stephen Waruru (KCB), beki Wilson Anekeya (Zoo), difenda Luke Ochieng (Western Stima) na kipa Brian Opondo (Kariobangi Sharks).

Wengine ni mvamizi Batts Awita (Nzoia Sugar), mshambuliaji Noah Wafula (hakuwa na klabu), Victor Ayugi (Vihiga United na KCB), kipa Edwin Mukolwe (Wazito FC) na Dennis Monda (Sofapaka). Anthony Gathu alitokea Murang’a Seal FC inayoshiriki NSL.

“Kampeni za Ligi Kuu si kibarua chepesi. Unahitaji wanasoka wenye uzoefu na tajriba katika kivumbi hicho. Ndiyo maana tumejinasia huduma za wanasoka 10 waliowahi kushiriki kivumbi hicho. Natarajia kwamba tutajivunia msimu wa kuridhisha baada ya wanasoka wapya kuoanisha mtindo wa kucheza kwao,” akasema Akhulia.

Wachezaji 11 ambao Bidco United wamesajili sasa wanafikisha idadi ya wanasoka kambini mwa kikosi hicho kuwa 30. Kwa mujibu wa Akhulia, hiyo ni idadi nzuri ya wachezaji ambao watabadilishana nafasi ipasavyo pindi uchovu na majeraha yatakapoanza kuwabishia.

Bidco United walijipata katika ulazima wa kujisuka upya baada ya kuagana na wachezaji tisa wakiwemo Frankline Mwenda, Eliud Emase, Elix Otieno, Collins Marita, Peter Mwangi, Castro Ogendo, John Oginga, Antony Kamau na Martin Mage.

  • Tags

You can share this post!

Dimbi la majitaka linavyohatarisha maisha ya wakazi wa...

Amonde na Injera kuongoza wanaraga watano wa Shujaa Bermuda