Michezo

Kocha wa Kayole alia ukosefu wa hela waponda kikosi chake

August 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

JOHN KIMWERE, NAIROBI

KOCHA wa Kayole Starlets, Joshua Sakwa inalitaka Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) lijitokeze na kufunguka kwamba halina fedha kuendesha kampeni za Ligi Kuu ya Wanawake (KWPL) pia Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza.

Kocha huyo amedokeza kuwa hatua ya FKF chini ya rais, Nick Mwendwa kutangaza kuwa itakuwa ikitoa fedha kiasi kwa klabu zote zinazoshiriki vipute hivyo ilifanya wahisani wao kuwakimbia.

”Binafsi ningeomba FKF itangaze kwamba haipo katika nafasi nzuri kutimiza ahadi ilitoa kwa klabu za vipute hivyo,” alisema na kudai kuwa imekuwa vigumu kwa wahisani kuwapiga jeki maana FKF iliwakikishia kutoa ufadhili kiasi kwa klabu zote.

Muhula huu Shirikisho la Duniani (FIFA) halijatoa ufadhili kwa vikosi hivyo kama lilivyotangaza. Baada ya FIFA kutoa tangazo hilo lilitoa Sh750, 000 msimu uliyopita pekee.

Kocha wa magolikipa wa Thika Queens akiongea na wachezaji hao kabla ya kuingia mzigoni kukabili Mathare United Women (MUW FC) kwenye mechi ya Ligi Kuu (KWPL) uwanjani Stima Club, Nairobi. Thika ilishinda mbao 2-1. Ukosefu wa ufadhili unaponda timu zinazoshiriki kipute hicho. Picha/ John Kimwere

Kayole Starlets imeibuka kati ya vikosi vinavyoteswa na ukata msimu na kuifanya kushindwa kusafiri ugenini mara mbili kushiriki mechi za kinyang’anyiro hicho. Ukosefu wa fedha umeifanya kuachia alama sita muhula dhidi ya Kisumu All Starlets na Vihiga Queens.

Akiongea muda mfupi baada ya kikosi hicho kuzaba Oserian Ladies mabao 3-1 kwenye mechi ya kirafiki, kocha huyo alisema kuwa ni vigumu sana wafuasi wao kugharamia nauli kwenda Magharibi mwa Kenya kutoka Nairobi ili kuwapigia debe.

Anaitaka FKF irejeshe mechi hizo kuchezewa viwanja vya mitaani ili kuvutia mashabiki.