Michezo

Kocha wa Kipande apania kuzika uzembe kikosini

October 1st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

KIPANDE FC imeshindwa kutamba mbele ya Kibagare Slums FC baada ya kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na kubahatika kutawazwa mabingwa wa Super Cup makala ya pili katika fainali zilizopigiwa uwanjani City Park, Nairobi.

Kocha wa Kipande FC, Hanningon Kimathi amesema kwa sasa anawazia mechi za kufukuzia Ligi ya Kaunti ya Nairobi muhula ujao.

Amedokeza kuwa baada ya kukiangalia kikosi chake analenga kuiweka safu ya ulinzi iwe bora baada ya kugundua inaruhusu magoli ya kizembe yanayoweza kumgharimu kwenye mechi za ligi.

”Tumetumia mashindano ya Super Cup mwaka huu kujifua ambapo la msingi tulipania kujifunza jinsi ya kufunga magoli mengi dhidi ya wapinzani wetu,” alisema kocha huyo na kuongeza kuwa tayari ametambua mapungufu ya vijana wake.

Kocha huyo amewatoa hofu wadau pia wafuasi wao na kuwaambia wasitie shaka mambo mazuri yanakuja.

Kipande FC ilitawazwa mabingwa wa ngarambe hiyo baada ya kuzoa kufunga magoli manne dhidi ya mabao ya Kibagare Slums.

Wachezaji wa Kipande FC waliungana na viongozi wa FKF Tawi la Nairobi Magharibi kusherekea baada ya kuibuka mabingwa Super Cup 2019. Picha/ John Kimwere

Kwenye mchezo wa mwisho, Kipande FC ilipata bao hilo kupitia Martin Kimathi. Kwenye mechi hizo, kabla ya kutoka nguvu sawa na Kibagare Slums ilitangulia kupepeta Zion Winners mabao 3-1.

Nao wasichana wa Kangemi Ladies waliibuka malkia wa kinyang’anyiro hicho baada ya kuzoa magoli mengi kuliko wapizani wao Patriots Queens.

Kangemi Ladies ya kocha, Joseph Orao iligonga Kibagare Girls mabao 3-0 kabla ya kuangukia pua ilipolazwa mabao 2-1 na Patriots Queens. Patriots Queens iliibuka nafasi ya pili baada ya kutoka sare tasa na Kibagare Girls kisha kuliza Kangemi Ladies mabao 2-1.

”Pia nashukuru wachezaji wangu maana wameanza kuonyesha mbinu tofauti tunazolenga kutumia muhula ujao tukipania kukazana kwa udi na uvumba kunasa tiketi ya kusonga mbele,” alisema kocha Kimathi.

Alipongeza baadhi ya wachezaji hao akiwamo Martin Kimathi, Francis Maina na Patrick Oluchili kwa kazi nzuri waliotenda kwenye michezo hiyo.

Kwenye mechi za mchujo Kundi C, Kipande ilimaliza kidedea kwa kukusanya alama saba sawa na Silver Bullets.

Nayo Kibagare Slums ilitwaa ubingwa wa Kundi B kwa kunasa alama mbili, sawa na WYSA United. Kundi A, Zion Winners iliibuka wababe kusajili pointi tatu, moja mbele ya Karura Greens.