Michezo

Kocha wa Mutomo akisifia kikosi chake

September 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

TIMU ya Mutomo FC ni kati ya Klabu zinazoyumbisha timu pinzani katika soka ya Aberdare Regional League, huku maskani yake ikiwa ni Gatundu Kusini, Kaunti ya Kiambu.

Kocha wake Peter Mburu, anasema vijana hao wameimarika ambapo hata timu kadha eneo la Aberdare na vitongoji vyake wana sababu ya kuhaha wakati wowote wanapokutana nao.

Timu hiyo ambayo hufanyia mazoezi katika Uwanja wa shule ya msingi ya Mutomo, Gatundu Kusini, inajivunia kuwa na kikosi dhabiti yenye nidhamu ya hali ya juu.

Katika mkondo wa kwanza wa mechi za Aberdare Regional League, timu hiyo iliweza kukamata nafasi ya sita na alama 42.

Kocha huyo nasema kikosi chake kiko imara na kuonyesha soka ya kuvutia mashabiki.

“Jambo linalonipa msukumo zaidi ni kujitahidi kuhakikisha mtizamo wa soka ya vijana hawa katika eneo la Gatundu unaonekana wa kushirikiana zaidi badala ya mgawanyiko,” anasema kocha huyo.

Kocha huyo pia anajivunia kuwa na vijana chipukizi wenye nidhamu huku kila mmoja akifuata maagizo yake.

“Vijana wangu wanapenda soka sana ishara kuwa wanadhamini vipaji vyao huku wakionyesha bidii bila kukata tamaa,” anasema Kocha Mburu..

Katika mechi ya hivi majuzi vijana hao waliiadhibu Muthiga FC kwa mabao 3-1 kwenye mechi ya kirafiki iliyopigiwa Uwanja wa Mutomo, Gatundu.

Huku timu hiyo ikijiandaa kucheza mechi ya Aberdare Regional League mwezi wa Septemba vijana hao wanaendelea kucheza mechi za kirafiki ili kujiweka imara.

“Tayari tumepata mwaliko katika mji wa Kiambu ili kucheza mechi ya kirafiki na Githunguri United FC. ili kujipima nguvu tukijiandaa kwa Ligi,” anasema Kocha huyo.

Anawashauri vijana kuzingatia nidhamu kama ngao yao ili waweze kupiga hatua kubwa katika uchezaji wa soka.

“Tukicheza mechi za kirafiki bila shaka tutakuwa na taswira nzuri kuhusu pahali uwezo wetu umefika,” asema.

Anasema kikosi chake cha wachezaji 28 kimekuwa imara na kuiletea timu sifa tele kwa muda wa zaidi ya miaka kumi mfululizo iicheza Ligi.

Hata hivyo kocha huyo anatoa wito kwa marefarii wawajibike msimu huu wa mwaka 2019 kwa kuchezesha mechi zao bila mapendeleo yoyote.