Michezo

Kocha wa Zamalek aungama kulemewa kupiga Gor

February 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA CECIL ODONGO

KOCHA Mkuu wa Zamalek SC Christian Gross amekiri kwamba walizidiwa mbinu na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini(KPL) Gor Mahia katika pambano la Jumapili, Februari 4, 2019 ugani MISC Kasarani.

Wapambe hao wa soka la Misri walizabwa mabao 4-1 na Gor Mahia katika mechi ya kwanza ya kundi D, kichapo ambacho hawakukitarajia kutokana na rekodi wanayojivunia dhidi ya K’Ogalo.

Hata hivyo, kocha huyo alisema ni mapema sana kuwahukumu na kusema wamebanduliwa kwenye mashindano hayo huku akiongeza kwamba mechi nyingi bado yapo ya kusakatwa na hawana lolote la kuwatia wasiwasi.

“Tulianza mechi zetu vibaya ila bado kuna mechi nyingi tutakazowajibikia. Tulikuwa na nafasi nzuri ya kushinda baada ya kutwaa uongozi lakini tulitoboka kirahisi na wakatumia nafasi hiyo kutuadhibu vikali,” akasema Gross.

Ingawa hivyo, mkufunzi huyo alikataa kulaumu mchezaji yeyote kutokana na matokeo hayo mabaya akisema yalichangiwa sana na uchezaji mbaya wa kikosi nzima.

“Ndiyo tulifanya makosa na kupoteza mechi lakini sitaki kumlamu mchezaji yeyote. Tulifanya vibaya haswa katika kipindi cha kwanza ndiyo maana siwezi kumtia lawamani mchezaji yeyote. Tuna mechi nyingine tunazojitayarishia kabla ya kukutana na Gor Mahia na lazima tuzishinde,” akaongeza Gross.

Zamalek wanaongoza msimamo wa jedwali la ligi ya Misri kwa alama 45, alama sita mbele ya nambari mbili Pyramids.