Koech na Chepchirchir wazolea Kenya sifa Sanlam Cape Town Marathon
Na GEOFFREY ANENE
KENYA imefagia mataji ya mbio za kilomita 42 za Sanlam Cape Town kupitia Edwin Kibet Koech na Celestine Chepchirchir nchini nchini Afrika Kusini mnamo Septemba 15, 2019.
Koech ametumia saa 2:09:20 kukamilisha umbali huo na kuwa mwanamume wa kwanza kutoka Kenya kunyakua taji hili baada ya Shadrack Kemboi mwaka 2015.
Chepchirchir pia ni Mkenya wa kwanza kushinda kitengo cha wanawake tangu Isabella Ochichi aibuke mshindi mwaka 2015.
Koech alimaliza kitengo chake sekunde 0.05 mbele ya Mkenya mwenzake Daniel Muindi (2:09:25) nao Mohamed Ziani (Morocco), Elroy Galant (Afrika Kusini) na Joseph Khoarahlane (Lesotho) wakafunga mduara wa tano-bora.
Chepchirchir alikata utepe kwa saa 2:26:44, muda ambao ni rekodi mpya ya wanawake ya Sanlam Cape Town Marathon baada ya kufuta rekodi ya mshindi wa mwaka 2018 Mnamibia Helalia Johannes (2:29:28). Chepchirchir amefuatwa kwa karibu na Waethiopia Nurit Shimels (2:27:40) na Gete Tilahun (2:28:32), mtawalia.
Nafasi tatu za kwanza ziliandamana na zawadi ya Sh1.8 milioni, Sh924,852 na Sh497,997, mtawalia. Chepchirchir aliongezwa Sh711,424 kwa kuweka rekodi hiyo mpya.
Makala haya ya 13 yalivutia zaidi ya watimkaji 7,000.