K’Ogalo walemea Ingwe tena Tusker ikipepeta Ulinzi
NA JOHN ASHIHUNDU
GOR Mahia wanaendeleza rekodi yao nzuri dhidi ya AFC Leopards walipoandikisha ushindi wa 1-0 mechi ya Ligi Kuu (KPL) iliyogaragazwa katika uwanja wa Nyayo, Nairobi mnamo Jumapili.
Mabingwa hao watetezi almaarufu K’Ogalo, walijipatia bao hilo muhimu kupitia kwa Austine Odhiambo aliyefunga kutokana na makosa ya kipa Levis Opiyo aliyejaribu kumchenga eneo la hatari kabla yake kumpokonya mpira.
Kutokana na ushindi huo, Gor wamefungua pengo la pointi tisa huku wakijivunia jumla ya pointi 57, mbele ya Police FC walio na 48, kila moja ikisalia na mechi tano kukamilisha ratiba ya msimu huu.
Katika mechi nyingine iliyochezewa Ulinzi Sports Complex, wenyeji Ulinzi Stars walichapwa 1-0 na Tusker ambao wamenata nafasi ya tatu baada ya kufikisha pointi 46.
Mjini Murang’a katika uwanja wa SportPesa Arena, Murang’a Seal waliagana sare tasa na Muhoroni Youth.
Bao la Tusker la ushindi lilifungwa na Erick Kapaito dakika ya 50, bao ambalo limepunguza kasi ya wanajeshi hao ambao sasa wanakamata nafasi ya 13 jedwalini.
Gor walimaliza mechi yao na wachezaji 10 baada ya kipa Kevin Omondi kulishwa kadi nyekundu kwa kumchezea ngware Victor Omune wa AFC, almaarufu Ingwe, akielekea langoni kufunga bao.
Mwamuzi aliamua penalti ipigwe, lakini kipa aliyeingia katika nafasi yake alizuia kombora la nahodha Clifton Miheso.
Mashabiki walishuhudia vitendo vya kushangaza miongoni mwa walinda usalama wa timu zote mbili waliotwangana kabla na hata baada ya mechi hiyo iliyovutia zaidi ya mashabiki 30,000.
Mashabiki wachache pia walionekana wakicharazana, lakini maafisa wa usalama waliwadhibiti huku mechi ikiendelea.
Hii ilikuwa mara mbili mfululizo kwa Gor Mahia kubwaga Leopards baada ya hapo awali kuibuka na ushindi wa 2-0 katika pambano la mkondo wa pili lililochezewa MISC, Kasarani.
Juhudi za Gor kupata bao la mapema zilizimwa na kipa Opiyo aliyeokoa hatari kadhaa langoni, zikiwemo mbili za Ronney Onyango na Bryson Wangai.
Benson Omala aliyetarjiwa kufunga bao ili kuimarisha rekodi yake alicheza kwa kiwango cha chini, kinyume na ilivyotarajiwa. Omala na Tito Okelo wa Police FC wanatoshana kwa ufungaji mabao, baada ya kila mmoja kucheza na nyavu mara tisa.