Michezo

KOMBE LAJA? Spurs waanza kuota taji baada ya kupiga hatua katika FA Cup

February 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

DELE Alli anaamini kuwa Tottenham Hotspur “inastahili kombe” inapolenga kumaliza ukame wa miaka 12 bila taji lolote.

Spurs ilisaidiwa pakubwa na Alli kupata magoli mawili ya mwisho katika dakika za lala-salama ikichabanga Southampton 3-2 Jumatano na kuingia raundi ya tano ya Kombe la FA.

Timu hii kutoka jijini London haijashinda taji tangu ibebe ubingwa wa kipute cha League Cup mwaka 2008.

“Tunastahili kushindia mashabiki wetu kitu,” alisema mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23. “Tunastahili kombe, ni muda mrefu sana. Hakuna atakayetupatia, kwa hivyo ni lazima tuzidi kutafuta mafanikio hayo.”

Mbali na kupoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Liverpool katika fainali ya Klabu Bingwa Ulaya mwezi Juni mwaka jana, Tottenham ilikamilisha Ligi Kuu ya msimu wa 2016-2017 katika nafasi ya pili na imeshiriki nusu-fainali ya mashindano mengine ya nyumbani kwa misimu mitatu mfululizo.

Vijana wa Jose Mourinho walijipata chini, mabao 2-1 dhidi ya Southampton katika mechi ya hiyo ya marudiano ya Kombe la FA, duru ya nne kabla ya Lucas Moura kusawazisha 1-1 dakika ya 78 na kisha Son Heung-min kufuma wavuni bao la ushindi kupitia penalti dakika ya 87 timu hiyo ikitinga raundi ya 16-bora.

“Inadhihirisha uwezo tulio nao,” aliongeza Alli.

“Timu yetu ni mojawapo ya timu bora duniani.”

Alli, aliyepata jeraha dogo katika ushindi wa Spurs wa mabao 2-0 dhidi ya Manchester City mnamo Jumapili iliyopita, alingizwa kama mchezaji wa akiba dhidi ya Southampton dakika ya 61. Alipigia Son pasi iliyozalisha bao la ushindi baada ya penalti kupatikana Son alipoangushwa ndani ya kisanduku. Hata hivyo, Spurs, ambayo ilikuwa na siku moja chache kujiandaa kuliko Southampton, ilikosa huduma za Harry Kane, Giovani lo Celso na Erik Lamela, wanaouguza majeraha, huku sajili mpya Steven Bergwijn akizuiwa na sheria kushiriki mchuano huo kwa sababu hakuwa katika mechi ya mkondo wa kwanza.

“Nadhani nilifanya vyema kwa sababu nilihitajika kutumia kikosi ambacho kina matatizo chungu nzima,” alisema Mourinho.

“Nilibadilisha mfumo kutoka walinzi watano hadi walinzi wanne wakati nilipohitaji kufanya hivyo. Kisha, Dele Alli ndiye alikuwa akiunganisha walinzi na safu ya ushambuliaji.

“Timu yangu ilifanya vyema. Kutokana na ukosefu wa wachezaji kadhaa, ilifanya kadri ya uwezo wake. Siku kadha zilizopita ilicheza soka nzuri sana.

“Tuliumia. Tulikutana na timu nzuri sana, timu ambayo ilikuwa nzuri uwanjani, lakini tulistahili kuibuka na ushindi. Walikuwa na wachezaji wao wazuri, walikuwa wamepumzika siku moja zaidi, walikuwa katika hali nzuri.

“Wachezaji walicheza kwa moyo wao wote. Mechi nne katika raundi mbili, ni kibarua kigumu sana kwa vijana wangu. Wanastahili furaha hii.”

Tottenham itakutana na Norwich katika raundi ijayo.

Ratiba: Chelsea na Liverpool, Tottenham na Norwich, Portsmouth na Arsenal, Leicester na Birmingham, Sheffield Wednesday na ManCity, West Brom na Newcastle, Derby na ManUnited, Reading na Sheffield United.