• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 10:55 PM
Komoro yapata motisha Kenya ikijiandaa kuingia AFCON 2021

Komoro yapata motisha Kenya ikijiandaa kuingia AFCON 2021

Na GEOFFREY ANENE

Huku Harambee Stars ya kocha Jacob ‘Ghost’ Mulee ikizamia maandalizi na wachezaji wake wa nyumbani, wanavisiwa wa Komoro wanazidi kupata motisha kambini mwao kabla ya ziara ya Nairobi.

Mshambuliaji El Fardou Mohamed Ben Nabouhane alifungia Red Star Belgrade mabao mawili na kuchangia pasi iliyozalisha bao timu hiyo kutoka Serbia ikilipua FC Slovan Liberec 5-1 katika mechi ya Ligi ya Uropa hapo Oktoba 29. Mchango huo wake umeshuhudia akitiwa katika orodha ya wawaniaji wa mchezaji bora wa wiki wa Ligi ya Uropa.

Anashindania tuzo hiyo dhidi ya Donyell Malen aliyefungia PSV Eindhoven kutoka Uholanzi magoli mawili ikilemea Omonia (Cyprus) 2-1, Michael Liendl aliyefungia Wolfsberger mabao matatu timu hiyo ya Austria ikikung’uta Feyenoord (Uholanzi) 4-1 na Elvis Manu aliyetingia Ludogorets (Bulgaria) mabao matatu ikipoteza 4-3 dhidi ya LASK (Austria).

“Mabao mawili na pasi iliyozalisha goli kutoka kwa El Fardou Ben Mohamed! Fomu hii nzuri kutoka kwa nahodha msaidizi wa timu ya taifa ya Komoro (Coelacanth) wiki mbili kabla ya kukabiliana na Kenya inatia moyo,” tovuti ya soka nchini Komoro ilisema.

Nabouhane, 31, ambaye pia ametajwa katika kikosi cha wiki cha Ligi ya Uropa, ndiye mfungaji wa mabao mengi ya Komoro (tisa).

Juma hili pia Komoro iliripoti habari nzuri kambini mwake ilipotangaza kuwa nahodha wa timu ya Guingamp nchini Ufaransa, Youssouf M’Changama amepona virusi vya corona. Kiungo Youssouf, ambaye anaongoza katika kuchezea Komoro mechi nyingi (32), pamoja na beki Chaker Alhadhur walipata virusi hivyo wakiwa nchini Tunisia kwa mechi za kirafiki. Mechi ya Komoro dhidi ya Tunisia Under-21 ilifutiliwa mbali kabla ya wanavisiwa hao kuduwaza Libya 2-1 mnamo Oktoba 11 katika mechi ambayo Youssouf alipachika bao la ushindi.

Kenya, ambayo inajivunia kupiga Komoro mara moja na kutoka sare mara mbili katika historia ya mataifa haya, pia inajivunia wachezaji wa kimataifa kama Michael Olunga (Japan), Victor Wanyama (Canada) na Eric Johanna Omondi (Uswidi). Mshambuliaji wa Kashiwa Reysol, Olunga anaongoza ufungaji wa mabao kwenye Ligi Kuu ya Japan. Wachezaji wa Kenya wanaosakata ughaibuni wanatarajiwa kuanza kuwasili kambini mnamo Novemba 2.

Harambee Stars na Komoro zitamenyana jijini Nairobi mnamo Novemba 11. Vijana wa Ghost watarudiana Novemba 15 ugenini. Mechi hizi ni za Kundi G za kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) 2021.

  • Tags

You can share this post!

Injera na wenzake kupimwa tena corona kabla ya kushiriki...

Ishara Guardiola ataungana upya na Messi Barcelona 2021