Kongamano la usimamizi sekta ya michezo laanza KU
Na LAWRENCE ONGARO
KONGAMANO la Maswala ya Michezo la The 4th International Conference of The African Sport Management Association (ASMA), limezinduliwa Alhamisi katika Chuo cha Mount Kenya.
Mkutano huo unalenga kuhamasisha umma umuhimu wa kujiweka timamu kiafya kwa msimamo wa (Mass Sports in Africa: Opportunities and Challenges).
Bw Japson Gitonga, Afisa mkuu katika Wizara ya Michezo aliyemwakilisha waziri alisema michezo katika bara la Afrika ni muhimu kwa sababu inaleta amani miongoni mwa wahusika wote na maendeleo kwa pamoja.
“Tunastahili kufanya michezo kuwa ya kitaaluma ambapo hatufai kuwaruhusu waigizaji kuingilia mchezo huo. Kuna watu wengi ambao wamejitolea kujihusisha na michezo lakini yastahili kuendeshwa na maafisa wenye ujuzi,” alisema Bw Gitonga.
Kongamano hilo litaendelea kwa siku tatu mfululizo hadi Jumamosi Aprili 6, 2019.
Limehudhuriwa pia na wageni zaidi ya 80 kutoka nchi kadha za bara Afrika kama Uganda, Tanzania, Nigeria, Ghana, Zimbabwe, na Kenya.
Lengo kuu ni kuwahamasisha wageni hao ili kuelewa kwa kina umuhimu wa kuendeleza michezo kwa utaratibu unaostahili na pia kuwa na wasomi wanaouelewa mchezo huo vyema.
Profesa Kihumbu Thairu, ambaye ni mhadhiri wa maswala ya afya ya kisaikolojia katika chuo kikuu cha Nairobi, alisema binadamu anastahili kufanya mazoezi hata mara tatu kwa wiki ili kuboresha hali yake ya kiafya kila mara.
” Iwapo mwanadamu atachukua nafasi yake kila mara angalau kufanya mazoezi, bila shaka atadumisha ukuaji wa afya yake kwa kiwango kikubwa. Hata mimi hapa mnionavyo kila asubuhi lazima nichukue muda wangu anagalau dakika 30 hivi kunyoosha viungo vyangu ili niwe sawa kiafya,” alisema Prof Thairu.
Alisema watoto wengi siku hizi wamezamia kutazama sinema za video mchana kutwa bila kunyorosha miili bila ya kuzingatia kwamba pengine wanahatarisha afya yao.
“Ningetaka kuwahakikishia kuwa utafiti unaonyesha ya kwamba watoto kutoka mashambani wako timamu kiafya kuliko wa mjini kwa sababu ya hali yao ya maisha.” alisema Prof Thairu.
Maisha marefu
Aliyekuwa wakati moja mwenyekiti wa Idara ya Masomo ya Kwata (Department of Physical Education), Bw Jonah Nyaga alitaja michezo kuwa muhimu kwa mwanadamu yeyote anayetamani kuishi maisha marefu.
“Iwapo ungetaka maisha yako yazidi kuwa marefu ni vyema kufanyisha mwili mazoezi kila mara,” alisema Bw Nyaga.
Afisa mkuu wa michezo ya Kenya Academy of Sports Bw Gordon Oluoch, alisema michezo hapa nchini haijapewa kipaumbele jinsi inavyostahili.
“Kila mara tunapozungumzia maswala ya michezo mambo ambayo huwasilishwa mbele ni ukosefu wa fedha, vifaa muhimu na wataalamu wanaostahili kuiendesha,” alisema Bw Oluoch.
Alisema licha ya kuwa katika mstari wa mbele katika michezo kwa miaka 30 bado Kenya inapitia changamoto ya utumizi wa dawa za kuongeza nguvu kwenye misuli.
Prof Peter Wanderi aliyewakaribisha wageni hao alitaka mkazo uwekwe katika michezo kwa lengo la kuleta amani na utangamano katika bara la Afrika na ulimwengu kwa jumla.