Michezo

Kosgei, Cheruiyot wafukuzia Sh22m Lisbon Half Marathon

March 16th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

MSHIKILIZI wa zamani wa rekodi ya dunia mbio za kilomita 42, Brigid Kosgei anapigiwa upatu kuibuka bingwa wa mbio za Lisbon Half Marathon mnamo Jumapili nchini Ureno.

Kuna bonasi ya Sh22, 477, 785 (Euro 150,000) kwa mshindi atakayevunja rekodi ya dunia.

Raia wa Uganda Jacob Kiplimo anashikilia rekodi ya dunia ya 21km ya wanaume baada ya kushinda jijini Lisbon kwa dakika 57:31 mwaka 2021.

Muethiopia Letesenbet Gidey ndiye mshikilizi wa rekodi ya dunia ya wanawake ya 21km baada ya kutawala Valencia Marathon nchini Uhispania kwa saa 1:02:54 mwaka 2021.

Rekodi za Lisbon Half zinashikiliwa na Kiplimo (57:31) na Mkenya Susan Chepkemei (65:44). Ziliwekwa mwaka 2021 na 2001, mtawalia.

“Nitajaribu kuandikisha muda wangu bora mpya ninapotumia Lisbon Half kujiandaa kwa mbio za London Marathon mwezi Aprili,” Kosgei anayejivunia muda bora wa dakika 64:49 katika nusu-marathon, akaambia waandalizi wa mbio hizo Ijumaa usiku.

Wakenya wengine jijini Lisbon ni pamoja na Vivian Cheruiyot (66:34), Betty Kibet (66:37), Pauline Esikon (67:15), Vivian Melly (67:35), Edith Jepchumba (30:53 katika 10km) na Abraham Kiptum (59:09). Pia kuna Brian Kwemoi (59:37), Bravin Kiptoo (59:37), Dominic Kiptarus (59:55), Dennis Kitiyo (61:06), Edward Zakayo (27:35.07 katika 10km), Geoffrey Kiboi (62:05) na Timothy Kipchumba (62:06).

Mbali na Kenya, kuna washiriki kutoka Ethiopia, Norway, Afrika Kusini, Amerika, Italia, Ujerumani, Morocco, Brazil, Jamhuri ya Ireland, Eritrea, Burundi, Ureno, Uhispania, Ecuador, Uingereza, Romania, Iran, Hungary, Estonia, Singapore, Urusi, Uswidi, Ufaransa, Mexico, Japan, Kazakhstan na Jamhuri ya Czech.