Michezo

KRA yafunga akaunti za benki za FKF kwa kulemewa kulipa ushuru

September 14th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na Geoffrey Anene

Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) limenyakwa na Mamlaka ya Kutoza Ushuru ya Kenya (KRA) kwa kutolipa malimbikizi ya ushuru wa Sh44 milioni.

Gazeti la Standard limeripoti Septemba 14, 2018 kwamba KRA imefunga akaunti za benki za FKF kutokana na deni hilo ambalo inasemekana afisi ya rais wa zamani Sam Nyamweya na rais wa sasa Nick Mwendwa zinanyosheana kidole cha lawama. “Hata hivyo, shughuli za FKF zinaonekana zinaendelea kama kawaida licha ya akaunti zake kufungwa.

Inasemekana kwamba Mwendwa sasa anatumia fedha zake kulipa timu ya taifa ya Harambee Stars. Septemba 9, 2018 alitoa mchango wake binafsi wa Sh2 milioni kuitunuku Harambee Stars kwa kushinda Ghana 1-0 katika mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2019,” gazeti hilo limedai.

Mbali na malimbikizi haya ya ushuru, FKF inakabiliwa na kesi zingine 11 zikiwemo mbili dhidi ya makocha wa zamani wa Harambee Stars Mbelgiji Adel Amrouche na Muingereza Bobby Williamson, ambao wanataka Sh66 milioni na Sh40 milioni mtawalia, kwa kufutwa kazi kinyume cha sheria.

Kesi hizi zinazua kumbukumbu za miamba wa soka wa Kenya Gor Mahia na AFC Leopards, ambao wamepitia ama wanapitia masaibu kama haya.

Mwezi Julai mwaka huu wa 2018, Gor iliripoti kwamba KRA imefunga akaunti zake kutokana na malimbikizi ya ushuru ya Sh129 milioni. Hiyo haikuwa mara ya kwanza Gor kujipata pabaya baada ya KRA kuibishia mlango mwaka 2014 ikitafuta ilipe Sh118 milioni.

Mwaka huo, mahasimu wa tangu jadi wa Gor, Leopards pia walifungiwa akaunti zao kutokana na malimbikizi ya ushuru wa Sh8 milioni.