Michezo

KRU yampa kocha Simiyu mikoba ya wanaraga wa Shujaa

September 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

INNOCENT ‘Namcos’ Simiyu amerejea kuwa kocha wa timu ya taifa ya wanaraga saba kila upande, Shujaa, baada ya Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) kumteua kuwa mrithi wa Paul Feeney – raia wa New Zealand aliyebanduka Juni 2020.

Akimtambulisha mkufunzi mpya kwa kikosi na mashabiki hapo jana, Mwenyekiti wa KRU, Oduor Gangla alisema Simiyu amepokezwa mkataba wa miaka miwili.

Uteuzi wa Simiyu unakamilisha sasa wiki nyingi za tetesi za kila sampuli kuhusu nani angepokezwa kiti moto cha Shujaa kati ya wakufunzi wanne waliounga orodha fupi ya mwisho. Mbali na Simiyu wengine waliokuwa wakiwania fursa ya kudhibiti mikoba ya Shujaa ni Dennis Mwanja, Paul Murunga na Nick Wakley ambaye ni mzawa wa Wales.

“Nina furaha kurejea kutia makali wanaraga wa Shujaa na ninajua ukubwa kazi iliyopo mbele na uzito wa kibarua kinachostahili kufanywa. Ni matumaini yangu kwamba tutashirikiana vilivyo na wadau wote kurejesha hadhi iliyojivuniwa na kikosi hapo zamani,” akasema Simiyu.

Simiyu alitimuliwa na KRU mnamo 2018 baada ya wanaraga wa Shujaa kuandamana kwa kuziba nembo ya Kenya kwenye jezi zao kulalamikia tukio la kutolipwa malimbikizi ya bonasi.

Kwa mujibu wa Gangla, Simiyu atakuwa huru kuteua maafisa atakaopendelea kufanya nao kazi kwenye benchi ya kiufundi. Kwa upande wake, Simiyu amekiri kwamba tayari ameafikiana na kocha atakayekuwa msaidizi ila akakataa kumtaja.

Awali, kocha Dennis Mwanja wa kikosi cha wanabenki wa KCB alikuwa akihusishwa pakubwa na uwezekano wa kupokezwa mikoba ya Shujaa baada ya kuungwa mkono na idadi kubwa ya wanachama wa Bodi ya KRU.

Japo Gangla alipinga, inaaminika kwamba KRU ilibadilisha msimamo katika dakika za mwisho na kumteua Simiyu badala ya Mwanja.

“Jopo lililoaminiwa na KRU kuendesha mahojiano liliafikiana kwa kauli moja kwamba Simiyu ndiye aliyekuwa mwaniaji bora zaidi kati ya wote waliotuma maombi ya kazi,” akasema Gangla kwa kufichua kwamba kati ya waliounga Jopo hilo ni Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa KRU, Thomas Odundo, kocha wa zamani wa Shujaa, Feeney na Peter Harding ambaye ni mshirikishi mkuu wa Shirikisho la Raga la Dunia (WR).

Simiyu, ambaye aliwatambisha Shujaa katika Raga ya Dunia mnamo 2018, alipokezwa mikoba ya timu ya taifa mnamo 2016 baada ya kumrithi Benjamini Ayimba.

Shujaa waliambulia nafasi ya 12 kwenye jedwali la Raga ya Dunia mnamo 2016-17 kwa kujizolea jumla ya alama 63. Walitinga nafasi ya nane kwa alama 104 katika msimu uliofuatia wa 2017-18 baada ya kuingia robo-fainali mara tano na kufuzu kuwania taji la Main Cup mara mbili katika duru za Canada na Hong Kong.

Katika enzi zake za uchezaji, Simiyu alivalia jezi za Shujaa mara 121 na kuwafungia jumla ya alama 321.

Baadhi ya wakufunzi ambao wamenoa Shujaa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita ni Mitch Ocholla (2011-12), Mike Friday wa Amerika (2012-13), Paul Treu wa Afrika Kusini (2014), Felix ‘Toti’ Ochieng (2015), Benjamin Ayimba (2016-17), Simiyu (2018) na Paul Murunga (2019).

Chini ya Feeney, Shujaa walifuzu kwa makala yajayo ya 32 ya Michezo ya Olimpiki na kukamilisha kampeni za Raga ya Dunia muhula huu wa 2019-20 katika nafasi ya 12 kwenye orodha ya timu 15. Kenya ilijizolea jumla ya alama 35 na kutinga robo-fainali za Main Cup mara mbili jijini Cape Town (Afrika Kusini) na Hamilton (New Zealand).

Feeney, ambaye pia aliongoza Kenya Morans kutinga fainali ya Tusker Safari Sevens mwaka jana, aliteuliwa kuwa kocha wa Shujaa mnamo Septemba 2019 baada ya mkataba wa Murunga kutamatika. Amewahi pia kunoa timu ya taifa ya Fiji na vikosi vya raga vya Auckland na Stormers nchini New Zealand na Afrika Kusini mtawalia.