Michezo

KRU yaunda kamati ya kuamua hatima ya msimu huu wa raga ya Kenya

May 31st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Raga la Kenya (KRU) limeunda kamati ya watu sita ambao wametwikwa jukumu la kutathmini mapendekezo ya washikadau kisha kuamua hatima ya kampeni za raga ya humu nchini msimu huu wa 2019-20.

KRU itawakilishwa na mkurugenzi wa ratiba za mechi Hillary Itela kwa pamoja na wanachama wa bodi Moses Ndale na Peris Mukoko.

Xavier Makuba wa KCB ataungana na wenzake Philip Jalango wa Kabras Sugar na George Mbaye wa Mwamba RFC kuwakilisha vikosi vya Ligi Kuu ya Kenya Cup.

Kwa mujibu wa Oduor Gangla ambaye ni mwenyekiti wa KRU, kamati hiyo itatoa ripoti itakayotoa uamuzi wa ama kurejelewa kwa kampeni za muhula huu au kufutiliwa mbali ka msimu wote baada ya kutalii hali mbalimbali.

“Kamati iliyoundwa itakuwa na wajibu wa kushauriana na wadau kisha kutoa fomula itakayowezesha kurejelewa kwa mapambano mbalimbali au kufutiliwa mbali kwa msimu wote baada ya kutathmini masuala tofautitofauti,” akasema bila kufichua muda ambao ripoti ya kamati inastahili kutolewa.

Iwapo mechi za raga zitarejelewa baada ya serikali kuondoa marufuku ya sasa yanayoharamisha mikusanyiko ya umma, basi hilo huenda likafanyika Julai kwa kuwa wachezaji watahitaji angalau kipindi cha kati ya wiki 6-8 kujiandaa.

KRU ilibatilisha maamuzi yake ya kufutilia mbali msimu mzima wa 2019-20 baada ya presha kutoka kwa klabu za Kenya Cup zilizotishia kutafuta haki mahakamani kwa madai kwamba zilikuwa zimewekeza kiasi kikubwa cha fedha kwa minajili ya kampeni za muhula huu.

Kabras wanaselelea kileleni mwa jedwali la Kenya Cup kwa alama 74, tatu zaidi kuliko KCB ambao ni wa pili. Homeboyz walitarajiwa kuvaana na Menengai Oilers kwenye nusu-fainali ya mchujo wa Kenya Cup na mshindi kupepetana na KCB. Kabras watavaana na mshindi kati ya Impala Saracens na Mwamba.

Strathmore Leos wanaoongoza jedwali la KRU Championship kwa alama 76 wanapania kurejea katika Ligi Kuu ya Kenya Cup baada ya kuwa nje kwa miaka miwili. Wasomi wa Chuo Kikuu cha Masinde Muliro (MMUST) wanashikilia nafasi ya pili kwa alama 67.