Michezo

KSG Ogopa FC yafika ilikolenga

August 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Kenya School of Government (KSG) Ogopa FC imetawazwa bingwa wa Ligi ya Kaunti ya Nairobi ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Tawi la Nairobi West msimu wa 2018/2019.

KSG Ogopa FC ilitwaa taji hilo baada ya wapinzani wao Maa FC kuingia mitini na kukosa kufika uwanjani kushiriki patashika ya fainali kutafuta bingwa wa kipute hicho.

Hata hivyo timu zote mbili, KSG Ogopa FC na Maa FC zimepandishwa ngazi kushiriki ngarambe ya Nairobi West Regional League (NWRL) msimu ujao.

”Licha ya kuzoa ushindi wa mezani baada ya wapinzani kusepa sina shaka kupongeza wachezaji wa kikosi changu kwa kuibuka mafahali wa kinyang’anyio hicho pia kutwaa tiketi ya kusonga mbele,” kocha wa KSG Ogopa FC, Peter Mutwiri alisema na kuongeza kuwa kufikia ufanisi huo haikuwa mteremko mbali kwa kuzingatia kampeni hizo zilishuhudia upinzani mkali tangia mwanzo.

”Bila shaka tunalenga kujituma mithili ya mchwa kupigania tiketi ya kupandishwa daraja msimu wa 2020/2021. Ninaamini vijana wa kikosi changu watajitahidi kadiri ya uwezo wao kukabili wapinzani wao ingawa nimegundua soka la kipute chochote hapa Kenya linazidi kuimarika kila mwaka huu,” alisema.

KSG Ogopa FC ilifuzu kushiriki ya kutafuta mshindi wa kipute hicho baada ya kunasa ubingwa wa mechi za Kundi B kwa kukusanya pointi 37, mbili mbele ya Kibera Soccer FC iliyomaliza katika nafasi mbili bora.

Nayo Maa FC iliyokuwa miongoni mwa vikosi vilivyotifua kivumbi kikali kwenye kampeni ngarambe hiyo iliwabwaga wapinzani wengine na kumaliza kileleni mwa Kundi A kwa kutwaa alama 45.

Nao wachezaji wa Uthiru Vision FC walitulia katika nafasi ya pili baada ya kuandikisha alama 42, nne mbele ya South B United Academy FC.

KSG Ogopa FC imepandishwa ngazi kushiriki kipute cha haiba ya juu ambapo lazima ijiweke tayari kupata ushindani mkali mbele ya washiriki wengine waliolemewa kunasa tiketi ya kusonga mbele.

”Kusema ukweli tunafahamu tunatarajia kukabili upinzani mkali kwenye kampeni za soka la kipute hicho,” kocha huyo alisema na kuongeza kuwa wamepania kukiongezea nguvu kikosi hicho ili kuhimili makali ya wapinzani wao.