Kukosekana kwa Mbio za Nyika kiini cha Wakenya kusuasua Diamond League – Kirwa
Na CHRIS ADUNGO
KUTOANDALIWA kwa mbio zozote za nyika hadi kufikia sasa kumechangia matokeo mseto yaliyosajiliwa na Wakenya kwenye duru mbili za ufunguzi wa kivumbi cha Wanda Diamond League.
Haya ni kwa mujibu wa kocha wa timu ya taifa ya riadha, Julius Kirwa ambaye ameshikilia kwamba mbio za nyika zimekuwa zikiwapa wanariadha wa humu nchini jukwaa mwafaka la kujiandalia kwa mashindano mbalimbali ya kimataifa kila msimu.
“Kihistoria, mbio za nyika zimekuwa zikiwapa Wakenya stamina na uthabiti wa kutamba katika mashindano yote mengine yanayofuatia kila msimu. Kutokuwepo kwa mbio hizo muhula huu kulichangia mseto wa matokeo yaliyoandikishwa na Wakenya jijini Monaco nchini Ufaransa na Stockholm, Uswidi,” akatanguliza.
Kilele cha msimu wa mbio za nyika mwaka huu kingekuwa kuandaliwa kwa kivumbi cha Afrika nchini Togo mnamo Aprili. Hata hivyo, janga la corona lilichangia kuahirishwa kwa mbio hizo mnamo Machi.
Bingwa wa dunia na Jumuiya ya Madola katika mbio za mita 5,000 Hellen Obiri alitawala fani hiyo kwenye kivumbi cha Diamond League jijini Monaco (14:22.12) kabla ya kuambulia nafasi ya 11 jijini Stockholm katika mbio za mita 1,500 kwa muda wa dakika 4:10.53.
Mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji, Beatrice Chepkoech aliibuka wa sita jijini Stockholm katika mbio za mita 5,000 kwa muda wa dakika 14:55.01 huku Ferguson Rotich akimaliza wa nne (1:45.11) katika mbio za mita 800.
Timothy Cheruiyot ambaye ni bingwa wa dunia katika mbio za 1,500 ndiye wa pekee aliyedumisha umahiri wake kwa kuibuka mshindi wa fani hiyo katika duru zote mbili za Diamond League.
Ingawa hivyo, Kirwa anaamini kwamba matokeo ya Wakenya yataimarika zaidi katika duru zilizosalia za Brussels, Ubelgiji (Septemba 4), Naples, Italia (Septemba 17), Doha, Qatar (Septemba 25) na China (Oktoba 17).
“Ni matumaini yetu kwamba corona itadhibitiwa vilivyo kufikia Oktoba ndipo tuanze msimu wa mbio za nyika hadi Februari 2021. Hilo litawapa wanariadha, hasa katika mbio za mita 5,000 na mita 10,000 jukwaa mwaridhawa zaidi la kujifua kwa Michezo ya Olimpiki jijini Tokyo, Japan,” akasema.
Wakati uo huo, bingwa wa Olimpiki katika mbio za mita 1,500, Faith Chepng’etich amesema atajaribu kuvunja rekodi ya mbio za mita 1,000 kwenye kivumbi cha Diamond League kitakachoandaliwa ugani AG Memorial Van Damme jijini Brussels mnamo Ijumaa.
Chepng’etich aliyekamilisha duru ya Monaco mnamo Agosti 14 kwa muda wa dakika 2:29.15, alisalia na nukta 17 pekee kufikia rekodi ya dunia ya dakika 2:28.98 iliyowekwa na Mrusi Svetlana Masterkova mnamo 1996.
“Sikujua jinsi nilivyokuwa karibu sana kuifikia rekodi hiyo. Ingawa ni kibarua kizito, sasa nitajaribu. Nina motisha, nimejiandaa vya kutosha na niko katika fomu nzuri,” akasema.
Nchini Ufaransa, Chepng’etich alitawala mbio za mita 1,000 na kumpiga kumbo Mwingereza Laura Muir (2:30.82) na Mageean Ciara wa Ireland aliyeambulia nafasi ya tatu (2:31.06).
Nyota huyo amekuwa akijifua katika eneo la Kaptagat kwa pamoja na bingwa wa dunia katika marathon Eliud Kipchoge na mshikilizi wa rekodi ya dunia katika nusu-marathon, Geoffrey Kamworor.
“Maandalizi yangu yamekuwa mazuri ila changamoto imekuwa ni kutokuwepo kwa uwanja maalumu wa kuniwezesha kukadiria kasi. Ingawa hivyo, napania kulenga juu zaidi,” akaongeza.
Mbio za Brussels zitakuwa za kwanza kwa mshikilizi wa rekodi ya dunia katika marathon ya wanawake, Brigid Kosgei kushiriki msimu huu. Kosgei atatoana jasho na bingwa wa dunia katika mbio za mita 10,000 na mita 1,500, Mholanzi Sifan Hassan katika juhudi za kuvunja rekodi ya dunia ya dakika 60 kwenye mbio za kilomita 18.517.