Kuondoka kwa Elneny kwaivua Arsenal nembo ya Uafrika
NA MWANGI MUIRURI
KLABU ya Arsenal inayojivunia ufuasi mkubwa barani Afrika ikitesa katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), sasa inaendelea kupoteza sura yake ya ‘Uafrika’ kwa kuwatema wachezaji weusi.
Timu hiyo ya Arsenal imekuwa kwa miaka mingi ikionekana kama sura ya Mwafrika kutokana na kusajili kwa wingi wachezaji wa kutoka mataifa ya bara la Afrika.
Lakini kocha Mikel Arteta licha ya kuendelea kuivisha vijana wake wa The Gunners, kiasi cha kufurahisha mashabiki duniani kote, kwa upande mwingine analaumiwa kwa kuruhusu Waafrika wa moja kwa moja kujiondoa kwa timu hiyo.
Licha ya mchezaji kama Bukayo Saka kuwa na asili ya Afrika, uraia wake rasmi ni wa Uingereza – nchi ya bara Ulaya.
Kwa sasa, hisia ziko juu mashabiki wakijiandaa kumuaga Mohamed Elneny ambaye ni raia wa Misri.
Elneny ametangaza kwamba anajiondoa ugani Emirates pasipo mnada wowote.
“Baada ya kuhudumia timu hii kubwa ya Arsenal kwa miaka minane, sasa wakati umewadia wa mimi kuondoka,” akasema kupitia mkanda wa video kwa mashabiki wake na wa Arsenal kwa ujumla.
Kuondoka kwa Elneny pia kuko sambamba na hali tete ya mchezaji Thomas Partey kutoka Ghana ambaye hatima yake katika timu hiyo haijulikani.
Elneny akiwa na umri wa miaka 31 sasa anaondoka Emirates akiwa amewajibikia Arsenal mara 161 na kutikisa nyavu mara sita.
Ujumbe wake kamili wa kuaga Arsenal na mashabiki ulisema “wenzangu wa Arsenal niko hapa leo kuwapasha ujumbe wa kwaheri na kuwashukuru kwa yote mema ambayo mmenitendea. Mapenzi yenu kwangu, kuniunga mkono na ukarimu wenu sitausahau kamwe”.
Alisema kwamba atawakosa na daima watasalia sehemu ya kumbukumbu rohoni mwake.
Ujumbe huo wa Elneny umewasononesha wengi, wengine wakitiririkwa na machozi.
Beki wakati wa Arsenal, William Saliba, alikimbia mitandaoni kujuta jinsi ambavyo yeye pia atamkosa.
“Sina maneno ya kukwambia jinsi ninavyotambua uwezo wako na jinsi ulivyo wa maana katika taaluma yangu. Ulinipokea vizuri ugan Emirates na ukaniunga mkono… Ndio maana ninasikitikia kuondoka kwako,” akasema.
Saliba alisema kwamba ataathirika Jumapili wakionana ana kwa ana kwa madhumuni ya kuagana rasmi.
Siku hiyo ndio michuano yote ya kutamatisha msimu wa EPL wa 2023/24 itachezwa na ambapo huenda Elneny akaondoka pasipo kutwaa taji hilo ambalo klabu ya Manchester City inapigiwa upatu kuponyoka nalo.
Ili Arsenal–ambayo ni ya pili kwa sasa na pointi 86–ilitwae, inatehemea pakubwa iadhibu Everton nayo Man City iliyo na pointi 88 ichapwe na West Ham United
Njia nyingine ya Arsenal kutwaa taji hilo ni kupitia sare ya Man City na West Ham nayo Everton ikubali kichapo cha The Gunners.