Kusogezwa kwa Olimpiki ni pigo kuu – Eliud
Na CHRIS ADUNGO
BINGWA wa Olimpiki Eliud Kipchoge amesema kwamba kuahirishwa kwa michezo hiyo iliyokuwa iandaliwe jijini Tokyo, Japan kati ya Julai 24 na Agosti 9, 2020, kumeyumbisha ndoto za wanariadha wengi kitaaluma.
Olimpiki za Tokyo 2020 ziliashirishwa na Kamati ya Kimataifa (IOC) hadi mwaka 2021 mnamo Jumanne baada ya presha kutolewa na wanariadha, makocha, mashirika, mashirikisho wanachama wa michezo hiyo na wadau mbalimbali kote duniani.
Hii ni mara ya pili kwa michezo hiyo ambayo imekuwapo kwa miaka 124 kuahirishwa. Mashindano hayo yaliwahi kufutiliwa mbali mnamo 1940 kutokana na Vita vya Pili vya Dunia.
Olimpiki ya mwaka huo ilikuwa pia iandaliwe jijini Tokyo. Kuahirishwa kwa Olimpiki, ambayo hufanyika kila baada ya miaka minne, ni nafuu kubwa Japan ambayo tayari imetumia mabilioni ya pesa kufanikisha maandalizi.
Virusi vya corona vinavyosababisha homa hatari ya Covid-19 vimefanya michezo mbalimbali kusimamishwa kote ulimwenguni. Jumla ya mataifa 189 yameathirika katika mabara yote isipokuwa Antarctica.
“Ni pigo kubwa kwa baadhi ya wanariadha, hasa wale ambao wamekuwa wakijifua mchana na usiku kwa minajili ya Olimpiki mwaka huu. Olimpiki ni mashindano muhimu sana miongoni mwa wanaridha wote duniani. Taaluma nyingi zimezimwa. Tukio hili la kuahirishwa kwa Olimpiki kumeathiri maisha mengi,” akatanguliza Kipchoge.
“Hakuna tukio lenye tija na fahari kubwa zaidi kwa mwanaridha yeyote kuliko hatua fupi ya kuvishwa medali shingoni baada ya kuibuka mshindi wa Olimpiki,” akasema Kipchoge huku akiwahimiza wanariadha wote walioathiriwa kwa namna moja au nyingine kukubali maamuzi ya vinara wa IOC na kuelekeza jitihada zao kukabiliana na virusi vya homa kali ya corona.
“Nawasihi waendelee kujiandaa kwa minajili ya mwaka ujao. Bado wana fursa. Kwa sasa itatulazimu kukubali mambo yalivyo na kupiga jeki juhudi zinazowekwa katika pembe mbalimbali za dunia,” akaongeza Kipchoge kwa kukiri kwamba azma yake kuu ni kutetea ubingwa wa taji la marathon katika Olimpiki za Tokyo.
“Hata hivyo, ilikuwa busara kuahirisha Olimpiki za mwaka huu hadi 2021. Natarajia kutetea ufalme wangu jijini Tokyo na kushuhudia mojawapo ya matukio ya kuridhisha zaidi katika makala hayo.”