KWAHERINI: Hazard aaga Chelsea baada ya ushindi
Na MASHIRIKA
BAKU, Azerbaijan
EDEN Hazard alipachika mabao mawili na kisha kukiri ilikuwa zawadi yake ya mwisho, huku Mbelgiji huyu akisaidia Chelsea kutawazwa wafalme baada ya kukanyaga Arsenal kwa mabao 4-1 katika fainali ya Ligi ya Uropa, Jumatano.
Mechi hii ilianza saa tano usiku Jumatano nchini Azerbaijan, lakini ilikuwa Alhamisi ilipopata msisimko baada ya milango ya magoli kufunguliwa na Olivier Giroud dakika ya 49 dhidi ya klabu yake ya zamani.
Hazard baadaye alimmegea pasi Pedro Rodriguez kuongeza bao la pili kabla ya kutikisa nyavu mara mbili ikiwemo kujaza penalti safi, huku Alex Iwobi akifungia Arsenal bao la kufutia machozi.
Mbelgiji Hazard anatarajiwa kuondoka Chelsea na kutua Real Madrid baada ya miaka saba nchini Uingereza, na ilikuwa njia nzuri sana ya kupatia klabu hiyo kwaheri.
“Nadhani ni kwaheri, lakini katika soka chochote chaweza kutokea,” alisema mchezaji huyu mwenye umri wa miaka 28. “Ndoto yangu ilikuwa kusakata soka katika Ligi Kuu ya Uingereza na nimefanya hivyo katika mojawapo ya klabu kubwa, kwa hivyo sasa ni wakati wangu wa kutafuta changamoto nyingine.”
Ni taji lake, na pia la Chelsea, la pili katika Ligi ya Uropa katika mwongo huu, na la kwanza kubwa kwa Maurizio Sarri kama kocha.
Chelsea, ambayo pia ilishinda taji hili mwaka 2013, itarejea katika Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao, lakini Arsenal bado itakuwa katika Ligi ya Uropa. Vijana wa Unai Emery walihitaji kuchapa Chelsea ili kufuzu, lakini hawakuwa na lao.
Emery alitarajia kushinda kombe hili kwa mara yake ya nne baada ya kulitwaa mwaka 2014, 2015 na 2016 akiwa Sevilla. Atapata fursa hiyo msimu ujao, lakini kwa sasa ukame wa miaka 25 wa Arsenal bila taji la mashindano yoyote ya Bara Ulaya unaendelea.
Chelsea itakumbuka Jumatano usiku kwa muda mrefu, sawa na Sarri, ambaye saa 24 kabla ya mechi aligonga vichwa vya habari alipoondoka uwanjani kwa hasira wakati wa mazoezi mbele ya kamera za runinga.
“Sarri ni kocha mzuri na anastahili ufanisi huu,” alisema beki David Luiz, ambaye ripoti zinadai anamezewa mate na Juventus.
Mashabiki 1,300 wa Chelsea waliofika jijini Baku hawatasahau usiku huo, ingawa kwa wale waliobaki Stamford Bridge watajutia.
Uamuzi wa Shirikisho la soka la Bara Ulaya (UEFA) kuruhusu fainali hiyo kuchezewa Baku umekashifiwa vikali, huku ugumu na gharama ya kuja katika ufukwe wa bahari ya Caspian zikizuia mashabiki wengi kusafiri. Pia, kiungo wa Arsenal, Henrikh Mkhitaryan hakuhudhuria mechi hiyo akihofia usalama wake.
Rais afika uwanjani
Rais wa Azerbaijan, Ilham Aliyev alikuwa miongoni mwa mashabiki waliofika uwanjani, lakini kulikuwa na maelfu ya viti ambavyo havikuwa na watu uwanjani Olympic, ambao ni wa karibu mashabiki 70,000,
Wachezaji walionekana kupoteza makali yao ya kawaida katika mechi hiyo iliyosakatwa majuma mawili na nusu baada ya Ligi Kuu kufikia tamati.
Hata hivyo, ilianza kuwa na mvuto, huku refa Gianluca Rocchi akipuuza Arsenal kutaka ipewe penalti baada ya Alexandre Lacazette kuanguka alipokabiliwa na kipa Kepa Arrizabalaga. Granit Xhaka kisha alishuhudia shuti lake kutoka mita 22 likiramba mwamba nusu saa ikikaribia.
Chelsea iliamshwa na shuti hilo, huku kipa Petr Cech akizuia kombora la Emerson Palmieri na kumnyima Giroud mwisho wa shambulio moja hatari.
Hata hivyo, Giroud aliweka Chelsea mbele mapema katika kipindi cha pili alipokamilisha krosi kutoka kwa Emerson.
Kutoka hapo, Chelsea ilisambaratisha Arsenal kwa kuongeza mabao kutoka kwa Pedro na Hazard aliyefuma penalti baada ya Ainsley Maitland-Niles kugonga Giroud na kupata bao lake la pili na la nne la Chelsea dakika ya 72. Nguvu-mpya Alex Iwobi alifungia Arsenal bao la kufutia machozi.