Kawangware wasalia wanafunzi katika darasa la gozi
JOHN ASHIHUNDU na JOHN KIMWERE
Matokeo mabaya yaliendelea kuandana Kawangware United baada ya kushindwa 2-0 na Dagoretti Former Players kwenye raundi ya 13 katika mechi ya Ligi Kuu ya Super 8 iliyochezewa Riruta BP Stadium, Jumapili.
Washindi walijipatia mabao yote kupitia kwa Mbusho Billy aliyefunga dakiika za 58 na 78th , matokeo ambayo yaliwawezesha kupanda hadi nafasi ya tano jedwalini kutokana na ushindi mara sita na sare moja.
Washindi ambao hupokea mafunzo kutoka kwa James Atieli wamejikusanyia jumla ya pointi 19 kufikia sasa.
Kawangware ambao mwenendo wao sio mzuri msimu huu, wamefikisha mechi tano bila ushindi, hali inayowaacha katika nafasi ya chini kwa point nane pekee, huku zikiwa zimesalia mechi mbili mkondo wa kwanza kumalizika.
“Tulianza kwa kiwango cha chini, lakini tukazidisha nguvu kadriri mechi ilivyoendelea. Bilas haka ushindi huu umetuweka katika nafasi nzuri wakati huu tunalenga kumaliza katika nafasi njema katikia mechi za mkondo wa kwanza,” alisema Atieli baada ya ushindi huo.
Kilikuwa kichapo cha pili mfululizo baada ya hapo awali kuchapwa 1-0 na Mathare Flames, matokeo ambayo naibu wa kocha Laban Mwangi alisema yamedidimiza matumaini ya timu yake kumaliza katika nafasi ya nzuri msimu huu.
“Tulicheza vizuri, lakini wapinzani wetu walipata nafasi na kuzitumia vyema. Hata hivyo, hatujakata tamaa.” Mwangi alisema.
Jericho All Stars walijipatia ushindi wa 2-0 dhidi ya Shauri Moyo katika mechi iliyochezewa Landi Mawe. Mabingwa hao watetezi wanaongoza msimamo wa ligi hiyo kwa 28 mbele ya Githurai All Stars (21) na NYSA (19).
Huruma Kona walishangaza mashabiki kwa kuibuka na ushindi wa 3-2 dhidi ya TUK 3-2 katika mechi iliyochezewa Huruma na sasa wamepanda hadi nafasi ya 11 kwa pointi 17, tatu mbele ya TUK wanaomiliki nafasi ya 14.
Matokeo kwa ufupi
Kawangware United 0-2 Dagoretti Former Players FC; Makadara Junior League SA 0-2 Meltah Kabiria
Team Umeme 1-1 NYSA; Shauri Moyo Sportiff 0-2 Jericho All Stars.
Mechi zifatazo zilitubuka kufuatia mvua kubwa iliyoharibu viwanja:
MASA na Githurai All Stars; Mathare Flames na Rongai All Stars; Lebanon FC na Metro Sports.