KWPL: Bullets yanyoa Ulinzi bila maji, Kibera ikinyeshea Nakuru
Na TOTO AREGE
KENYA Police Bullets waliendelea kutawala Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL) baada ya kuwanyoa bila maji Ulinzi Starlets kwa kuwatandika 4-0 katika uwanja wa Police Sacco, Nairobi mnamo Jumamosi.
Bullets sasa wana jumla ya alama 34 wakiwa juu katika msimamo wa ligi na wamefungua mwanya wa alama tano baada ya mechi 15 za ligi.
Winga Puren Alukwe alikuwa wa kwanza kucheka na nyavu katika dakika ya kwanza kabla ya mshambulizi Rebecca Okwaro kufunga bao la pili la klabu hiyo dakika ya 19. Akukwe alirudi tena na bao la dakika ya 46 huku nguvu mpya Chris Kach akimaliza kazi ya ziada na bao la nne dakika za lala salama kipindi cha pili.
Kufikia sasa Okwaro ndiye mfungaji bora wa ligi hiyo akiwa na mabao 11.
Ulinzi wanasalia katika nafasi ya pili na alama 29. Mabingwa watetezi Vihiga Queens wanafuata katika nafasi ya tatu na alama 28 wakiwa na mechi mbili za ziada ambazo huenda zikawavunia alama.
Bullets sasa wanahitaji ushindi mmoja pekee katika mechi zilizosalia kutwaa ubingwa wa ligi. Mechi zilizosalia ni dhidi ya Bunyore Starlets na Kibera ugenini na Zetech Sparks nyumbani.
Wameandikisha rekodi ya kutopoteza mechi msimu huu na pia hawajapoteza mechi yoyote nyumbani.
Ugani The Wolves Den mjini Olooloitikosh katika Kaunti ya Kajiado, Kibera Girls Soccer iliwanyeshea Nakuru City Queens FC 3-0. Mabao hayo yalitiwa kimiani na Cynthia Atieno, Mmboga Lilian na Liambila Mariaa katika dakika za 49, 60 na 85 mtawalia.
Kibera waliendelea kusalia katika nafasi ya nne na alama 27 nao Nakuru wakiganda katika nafasi ya tisa na alama 14.
Matokeo ya Jumamosi
Kenya Police Bullets 4-0 Ulinzi Starlets
Kibera Girls Soccer 3-0 Nakuru City Queens
Jumapili
Soccer Assassins FC vs Bunyore Starlets FC (Mumboha Grounds, Luanda 12pm),
Bungoma Queens FC vs Zetech Sparks FC (Sang’alo Institute, Bungoma 1pm).