Lampard aahidi kufanya makuu usukani Chelsea
Na MASHIRIKA
LONDON, Uingereza
FRANK Lampard ameahidi kuendelea kufanya Chelsea kuwa ‘mshindani halisi’ kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya klabu hiyo kuthibitisha kumwajiri rasmi kama kocha wake kwa kandarasi ya miaka mitatu Alhamisi.
Lampard alinyakua mataji 13 katika miaka 13 na kuwa mfungaji bora wa Chelsea baada ya kupachika mabao 211 kutokana na mechi 648 ugani Stamford Bridge.
Hata hivyo, kiungo huyo wa zamani wa Uingereza amefanya kazi ya ukocha kwa mwaka mmoja pekee alipoongoza Derby County kufika fainali ya Ligi ya Daraja ya Pili mwezi Mei lakini wakalemewa na Aston Villa.
Lampard anakabiliwa na kile alichotaja kama changamoto kubwa katika taaluma yake na Chelsea, iliyopoteza mchezaji wake bora Eden Hazard aliyejiunga na Real Madrid mwezi Juni.
Pia, hawezi kusajili wachezaji wapya kwa sababu klabu hii inatumikia marufuku ya kutonunua wachezaji kwa vipindi viwili vya uhamisho baada ya kuvunja sheria za Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).
Hata hivyo, anaamini Chelsea bado inaweza kusalia mshindani mkali wa nafasi nne za kwanza kwenye EPL.
“Tunataka kushiriki soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kila mwaka. Nadhani hiki ni kitu kinachostahili kutuchochea. Tunataka kukuza wachezaji na kusalia na ushindani,” alisema Lampard.
“Bila shaka kuna vitu vinavyoweza kufanya tutimize haya ama la kama marufuku dhidi ya kusajili wachezaji. Tunafahamu Manchester City na Liverpool walituacha na mwanya mkubwa wa alama msimu uliopita na hatufai kujidanganya kuhusu hilo, lakini si vizuri kuacha kujaribu kuwa kileleni na nadhani tunastahili kuwa juu.”
Lampard anajaza nafasi ya Mwitaliano Maurizio Sarri, ambaye aliondoka Uingereza mwezi uliopita kuchukua mikoba ya kunoa Juventus. Sarri aliongoza Chelsea kurejea katika soka ya UEFA msimu ujao, 2019-2020 na pia akashinda Ligi ya Uropa katika msimu mmoja aliokuwa uwanjani Stamford Bridge.
Hata hivyo, Sarri hakupendwa na mashabiki kutokana na mbinu zake na pia kusita kuchezesha baadhi ya wachezaji chipukizi wa Chelsea waliovutia.
Kuteuliwa kwa Lampard kunalenga kurekebisha uhusiano huu na mashabiki.
“Frank anajua klabu hili na kuielewa, na msimu uliopita, alidhihirisha kuwa yeye ni mmoja wa makocha wachanga walio na talanta katika soka,” alisema Mkurugenzi wa Chelsea, Marina Granovskaia.
“Baada ya miaka 13 akituchezea na kuwa shujaa wa klabu hii na mshikilizi wa rekodi ya mfungaji bora, tunaamini muda huu ni mzuri kwake kurejea hapa na tunafurahia kuwa amejiunga nasi.”
Lampard alielekea Derby na wachezaji wawili Fikayo Tomori na Mason Mount kutoka Chelsea kwa mkopo na waling’ara.
Naibu wake Jody Morris pia anafahamu Chelsea nje-ndani baada ya kuwa muhimu katika akademia ya klabu hii kabla ya kujiunga na Lampard katika klabu ya Derby mwaka 2018.
“Kile tunacho hapa tayari ni kikosi imara na tuna wachezaji walio na umri mdogo ambao bado hajafikia viwango vyao, lakini baadhi yao wameonyesha uwezo wao katika timu ya kwanza,” alisema Lampard.
Hata hivyo, anakabiliwa na kibarua kigumu katika mechi zake mbili za kuanza msimu dhidi ya Manchester United kwenye Ligi Kuu na soka ya UEFA Super Cup dhidi ya mabingwa wa Ulaya, Liverpool.