Michezo

Lampard asifu mmiliki wa Chelsea kuimarisha klabu

March 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

KOCHA Frank Lampard wa Chelsea, amempongeza mmiliki wa klabu hiyo Roman Abrahimovich na Mkurugenzi wa Michezo, Marina Cranovskaia kwa juhudi zao za kujaribu kuirejesha klabu hiyo kwenye ubora wake.

“Katika miaka ya karibuni, timu za Manchester City na Liverpool zimeweka viwango bora ligini na sisi pia sharti tujitolee, hasa baada ya marufuku ya kutuzuia kusajili kuondolewa,” alisema kiungo huyo mstaafu ambaye pia aliwahi kuchezea klabu hiyo ya Stamford Bridge.

“Nafurahia ninapozungumza na bodi na kuungwa mkono, wakati huu tunapigania kumaliza miongoni mwa nne bora msimu huu,” alisema Lampard ambaye alishinda mataji matatu ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) akiwa na Chelsea.

“Kwa sasa juhudi za kuwania ubingwa wa EPL zimekumbwa na changamoto kubwa, lakini tutajiandaa na kujaribu tena msimu ujao baada ya kusajili wachezaji kadhaa wapya,” aliongeza.

“Kiwango chetu kimeshuka kwa kiwango fulani. Sioni upinzani uliokuwepo miaka ya hapo nyuma tuliporaruana vilivyo na timu kama Manchester United, wakati tulipokuwa tukishika nafasi ya kwanza au ya pili katikati ya miaka ya 2000.”

“Chelsea si vile ilivyokuwa wakati wetu na akina John Terry. Lazima turejee pale kwa ajili ya kuwafanya mashabiki wajivunie kila wakati tunapocheza na kujaribu kushinda mechi nyingi kadiri inavyowezekana,” aliongeza Lampard ambaye alikuwa naibu nahodha wa Terry.

Wakati huo huo, kipa Kiko Casilla wa Leeds United amefungiwa kucheza mechi nne na kupigwa faini ya Sh7.5 milioni kwa kutoa lugha ya ubaguzi dhidi ya Johnathan Leko wa klabu ya Charlton.

Leko anayechezea Leeds kwa mkopo akiwa mali ya West Brom alifanya kitendo hicho baada ya timu yake kuibwaga Charlton 1-0 katika mechi iliyochezewa uwanja wa Valley.

Baada ya uchunguzi wa kina, kipa huyo alihukumiwa na Chama cha Soka Uingereza (FA), ingawa amekanusha tuhuma hizo kupitia kwa mtandao wa klabu yake ya Leeds.

Casilla amesema hana kosa na kusema kwamba kipindi cha miezi mitano iliyopita maisha yake ya soka yamekuwa magumu zaidi.

“Nitaheshimu hatua ya FA kuhusu tuhuma za kiubaguzi. Naunga mkono vita dhidi ya ubaguzi wa rangi michezoni.”