Michezo

Leeds United wampata kiungo Michael Cuisance kutoka Bayern Munich

October 1st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

LIMBUKENI wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Leeds United, wamejinasia maarifa ya kiungo wa Bayern Munich, Michael Cuisance.

Chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 21 amewahi kuchezea kikosi cha makinda wa Ufaransa. Alihamia Bayern mnamo Agosti 2019 baada ya kushawishiwa kuagana na Borussia Monchengladbach ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kwa kima cha Sh1.4 bilioni.

Cuisance aliwajibikia Bayern ambao ni wafalme wa Bundesliga na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) katika msimu wa 2019-20 na akawafungia bao moja.

Alitokea benchi katika kipindi cha pili katika ushindi wa 8-0 uliosajiliwa na Bayern dhidi ya Schalke katika mechi ya kwanza ya Bundesliga msimu huu.

Cuisance alikuwa mchezaji wa akiba ambaye hakutumiwa katika gozi la Uefa Super Cup lililowakutanisha Bayern na Sevilla mnamo Septemba 24, 2020. Hata hivyo, aliachwa nje ya kikosi kilichotegemewa na kocha Hansi Flick katika mechi ya Bundesliga iliyoshuhudia Bayern wakipokezwa kichapo cha 4-1 kutoka kwa Hoffenheim mnamo Septemba 27, 2020.

Cuisance alisalia benchi katika fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) iliyoshuhudia Bayern wakizamisha chombo cha Paris Saint-Germain (PSG) kwa bao 1-0 jijini Lisbon, Ureno mnamo Agosti 23, 2020.

Cuisance anakuwa mchezaji wa tano kusajiliwa na Leeds United ya kocha Marcelo Bielsa hadi kufikia sasa muhula huu. Kikosi hicho kimesajili pia wanasoka Rodrigo Moreno (Sh3.6 bilioni) kutoka Valencia, Diego Llorente (Sh2.5 bilioni) kutoka Real Sociedad, Robin Koch (Sh1.8 bilioni) kutoka Freiburg na aliyekuwa fowadi wa zamani wa Wolves, Helder Costa (Sh2.2 bilioni).

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO