Michezo

Leeds United wasajili Llorente kutoka Real Sociedad

September 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

LEEDS United wamemsajili beki Diego Llorente, 27, kwa mkataba wa miaka minne kutoka Real Sociedad kwa kima cha Sh2.5 bilioni.

Mhispania huyo anatarajiwa kutoa ushindani zaidi kwa madifenda Robin Koch, Liam Cooper na Pascal Struijk.

Llorente ambaye pia amewahi kuchezea Real Madrid ya Uhispania anaweza pia kutamba katika safu ya kati.

Kutua kwake Leeds United ambao wanashiriki Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu kwa mara ya kwanza baada ya miaka 16, kunamfanya kuwa sajili wa nne wa kikosi hicho muhula huu.

Chini ya kocha Marcelo Bielsa, Leeds United wamejinasia huduma za fowadi Rodrigo Moreno kutoka Valencia kwa kima cha Sh3.6 bilioni na winga wa zamani wa Wolves, Helder Costa aliyejiunga nao kwa Sh2.2 bilioni.

Koch aliingia katika sajili rasmi ya Leeds United kwa Sh1.8 bilioni baada ya kuagana na Freiburg ya Ujerumani.

“Ilikuwa vigumu kufikia maamuzi ya kuondoka Sociedad kwa pamoja na familia yangu. Hata hivyo, naamini kwamba nilifanya maamuzi bora zaidi kwa minajili ya makuzi yangu kitaaluma,” akasema Llorente.

Sogora huyo ambaye amechezea timu ya taifa ya Uhispania katika jumla ya mechi tano, atavalia jezi nambari 14 kambini mwa Leeds United.

Kufikia sasa, Leeds United wamefunga jumla ya mabao saba katika mechi mbili za ufunguzi wa kampeni za EPL msimu huu wa 2019-20.

Walipiga 4-3 na mabingwa watetezi Liverpool katika mchuano wa ufunguzi wa msimu mnamo Septemba 12 kabla ya kuwapepeta Fulham 4-3 katika mchuano wa pili mnamo Septemba 19, 2020.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO