Leicester kujinasia fowadi matata wa Uturuki, Cengiz Under kutoka AS Roma
Na MASHIRIKA
KOCHA Brendan Rodgers amethibitisha kwamba Leicester City wako katika hatua za mwisho za mazungumzo na AS Roma kuhusu uwezekano wa kujitwalia huduma za fowadi Cengiz Under, 23.
Nyota huyo raia wa Uturuki alijiunga na Roma ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) mnamo Julai 2017 baada ya kuagana rasmi na Istanbul Basaksehir.
Tangu wakati huo, Under amechezea Roma katika jumla ya mechi 88 kwenye mashindano yote na akafunga mabao 17.
“Ni mwanasoka mzuri sana. Mazungumzo kati ya Leicester na Roma yako katika hatua muhimu na dalili zote zinaashiria kwamba Under atakuwa mchezaji wetu wakati wowote wiki hii,” akatanguliza Rodgers.
“Tunahitaji mvamizi mwenye kasi ya juu zaidi ambaye pia amejaliwa kipaji cha kupiga chenga na kuchangia mabao katika safu ya mbele. Mwenye uwezo huo kwa sasa ni Under ambaye sina shaka atajiunga nasi,” akaongeza.
Kati ya sababu zilizochochea Leicester kumvizia Under ni hofu kuhusu uwezekano wa kumpoteza fowadi Demarai Gray, 24, ambaye amekataa kutia saini mkataba mpya licha ya kusalia na mwaka mmoja pekee kwenye kandarasi yake ya sasa na mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2015-16.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO