• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Leicester wafundisha Spurs kusakata soka ya EPL kwa kuipokeza kichapo cha 2-0

Leicester wafundisha Spurs kusakata soka ya EPL kwa kuipokeza kichapo cha 2-0

Na MASHIRIKA

KOCHA Brendan Rodgers wa Leicester City amesisitiza kwamba wanasoka wake “hawatajinaki kupita kiasi na kujisahaulisha majukumu yaliyoko mbele yao” licha ya kuwaangusha majabali Tottenham Hotspur mnamo Jumapili na kupaa hadi nafasi ya pili kwenye jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Leicester walishuka dimbani kwa minajili ya mchuano huo wakishikilia nafasi ya nne jedwalini huku Spurs ya kocha Jose Mourinho ikishikilia nafasi ya tatu kwa alama 25.

Jamie Vardy aliwafungia Leicester bao la kwanza kupitia penalti ya dakika ya 45 kabla ya Toby Alderweireld kujifunga katika dakika ya 59.

Ushindi huo wa Leicester uliwapaisha hadi nafasi ya pili kwa alama 27, nne pekee nyuma ya mabingwa watetezi Liverpool waliotua kileleni mnamo Jumamosi baada ya kutandika Crystal Palace 7-0 uwanjani Selhurst Park mnamo Disemba 19.

“Wanasoka wa Leicester wamejitahidi kufanya kazi nzuri kufikia sasa msimu huu. Licha ya majeraha mengi, kikosi kilichosalia kimetuwakilisha vyema katika soka ya Europa League na hata EPL. Vijana wanacheza kwa kujiamini sana na wamepania kutumia vizuri fursa chache wanazozipata katika kila mechi kufunga mabao muhimu,” akasema Rodgers.

“Malengo yetu yako wazi kwa mashabiki kwa kuwa tunataka kuwa miongoni mwa wagombezi halisi wa ubingwa wa EPL msimu huu japo idadi kubwa ya wanasoka wetu ni chipukizi tu.”

“Tutaona jinsi mambo yalivyo japo narishishwa sana na hatua kubwa ambayo kikosi kizima imepania kupiga. Tunachohitaji sasa ni kuimarisha makali ya safu ya kati kwa kusajili kiungo mpakuaji atakayeshirikiana vilivyo na James Maddison,” akaongeza kocha huyo.

Penalti iliyofungwa na Vardy mwishoni mwa kipindi cha kwanza ilitokana na tukio la Serge Aurier wa Spurs kumpiga kumbo Wesley Fofana ndani ya kijisanduku. Tukio hilo lilithibitishwa na refa Craig Pawson aliyelazimika kurejelea video ya tukio hilo kwenye mtambo wa teknolojia ya VAR.

Goli la pili la Leicester waliotawazwa mabingwa wa EPL mnamo 2015-16, lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati ya Maddison, Vardy na Marc Albrighton.

Ingawa Son Heung-min na Harry Kane walielekeza fataki nyingi kwenye lango la Leicester, kipa Kasper Schmeichel alisalia makini na akazidhibiti vilivyo.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Leicester kushinda Spurs ugenini katika gozi la EPL tangu 2015-16 ambapo walisajili ushindi wa 1-0

Tottenham kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Stoke City kwenye robo-fainali za League Cup mnamo Disemba 23 kabla ya kuwaendea Wolves katika EPL ugani Molineux mnamo Disemba 27. Kwa upande wao, Leicester watakuwa wenyeji wa Manchester United ugani King Power katika mchuano wa EPL mnamo Disemba 26.

You can share this post!

Raila atakuwa rais wa tano wa Kenya – Wabunge

Watford wampa Xisco Munoz mikoba yao ya ukocha