Michezo

Leicester City yaambiwa 'lenga 4-bora'

October 1st, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

KOCHA Brendan Rodgers wa Leicester City amekiri kwamba kubwa zaidi katika maazimio yao ni kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ndani ya mduara wa nne-bora mwishoni mwa msimu huu.

Ingawa hivyo, amewataka vijana wake kujihadhari dhidi ya kupotezwa dira na sifa tele wanazomiminiwa na vyombo vingi vya habari ambavyo tayari vimeanza kuwahusisha na uwezekano wa kunyanyua ubingwa wa EPL kwa mara nyingine muhula huu. Jamie Vardy alifunga mabao mawili na kuwaongoza waajiri wake Leicester City kuwaponda Newcastle United 5-0 mwishoni mwa wiki jana uwanjani King Power.

Ni ushindi ambao uliwapaisha Leicester hadi nafasi ya tatu jedwalini na hivyo kuwaaminisha zaidi kuwa wana uwezo wa kurejesha kumbukumbu za 2015-16 walipotawazwa wafalme chini ya mkufunzi Claudio Ranieri. Ushindi huo ndio mnono zaidi kuwahi kusajiliwa na Leicester katika historia yao ya kushiriki kivumbi cha EPL.

Kufikia sasa, Leicester wanajivunia alama 14, tatu zaidi kuliko Chelsea, Tottenham, Bournemouth na Crystal Palace ambao kwa sasa wanfunga mduara wa tisa-bora. Ingawa hivyo, ni pengo la alama saba ndilo linalotamalaki kati ya Leicester na Liverpool wanaoselelea kileleni mwa jedwali.

 

Baadhi ya wanasoka wa Leicester City washerehekea baada kufunga bao la tatu katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza dhidi ya Newcastle United uwanjani King Power mjini Leicester, Uingereza, Jumapili, Septemba 29, 2019. Picha/ AFP

Mabingwa watetezi Manchester City wanashikilia nafasi ya pili kwa alama 16 chini ya kocha mzawa wa Uhispania, Pep Guardiola.

Mabao mengine ya Leicester yalifumwa wavuni kupitia kwa Ricardo Pereira, Wilfred Ndidi na Paul Dummett aliyejifunga baada ya kujaza kimiani mpira kutoka kwa Dennis Praet wa Leicester City.

Leicester kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Liverpool mwishoni mwa wiki hii katika mchuano utakaomshuhudia kocha Rodgers akirejea ugani Anfield kwa mara ya kwanza tangu atimuliwe na Liverpool mnamo 2015 na nafasi yake kupokezwa Jurgen Klopp aliyewachochea kunyanyua ufalme wa UEFA msimu jana na kumaliza kampeni za EPL katika nafasi ya pili.

Kwa upande wao, Newcastle watawaalika Manchester United uwanjani St James Park.