Michezo

Leicester yapiga msumari kwenye jeneza la Pellegrini

December 30th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

KLABU ya Leicester ilitia kikomo enzi ya Manuel Pellegrini kama kocha mkuu wa West Ham baada ya kuilima 2-1 uwanjani London, Jumamosi.

Pellegrini aliingia katika mchuano huo akikodolea macho kuachishwa kazi kutokana na msururu wa matokeo duni. Alitimuliwa dakika 10 baada ya mechi hiyo kutamatika.

Leicester ilifanyia kikosi chake kilicholipuliwa na Liverpool 4-0 mnamo Desemba 26 mabadiliko tisa.

Mshambuliaji Jamie Vardy, ambaye amepata mtoto wa kike, alikuwa katika orodha ya wachezaji walioachwa nje, huku Kelechi Iheanacho na Demarai Gray wakitumia vilivyo fursa nadra ya kuanza mechi ligi kwa kufunga bao moja kila mmoja.

“Wakati wowote unapopata fursa kama hii baada ya kukosa kuchezeshwa mara kwa mara ni muhimu kuitumia vyema,” alisema Gray, ambaye pia alishuhudia penalti yake ya mapema ikipanguliwa na kipa Lukasz Fabianski.

Leicester almaarufu Foxes ilipunguza mwanya kati yake na viongozi Liverpool hadi 10, ingawa vijana hawa wa kocha Brendan Rodgers wamesakata mechi mbili zaidi ya vijana wa Jurgen Klopp.

Foxes wanashikilia nafasi ya pili. Wamepata nafasi ya kupumua baada ya kufungua pengo la alama nne dhidi ya mabingwa watetezi Manchester City.

Jumapili vijana wa Pep Guardiola walimenyana na Sheffield United na kupata ushindi wa mabao 2-0.

Pablo Fornals alisawazishia West Ham 1-1 kabla tu ya dakika 45 kukatika, lakini kichapo cha saba katika mechi tisa zilizopita kiliweka West Ham alama moja nje ya mduara hatari wa kutemwa.

“Ni wazi kuwa tulihitaji mabadiliko ili kurejesha klabu katika njia inayofaa na sawa na maazimio yetu ya msimu huu,” alisema mwenyekiti wa West Ham, David Sullivan.

“Tulihisi ni muhimu kuchukua hatua wakati huu ili kupatia kocha mpya muda mzuri wa kujaribu kutimiza lengo hilo.”

Kocha wa sita kufurushwa

Pellegrini ni kocha wa sita kufurushwa msimu huu kwenye Ligi Kuu ya Uingereza baada ya Marco Silva (Everton), Quique Flores (Watford), Unai Emery (Arsenal), Mauricio Pochettino (Tottenham) na Javi Gracia (Watford).

Baadhi ya makocha wanaosemekana wamo mbioni kuchukua nafasi ya Pellegrini ni David Moyes, ambaye aliondoka West Ham mwaka 2018 baada ya kuiongoza kukwepa kuangukiwa na shoka, kocha wa zamani wa Brighton Chris Hughton na kocha wa zamani wa Middlesbrough Tony Pulis.

Leicester iliingia mchuano huo bila ushindi katika mechi tatu zilizopita baada ya kutoka 1-1 dhidi ya Norwich na kisha kupepetwa 3-1 na Manchester City na kuabishwa 4-0 dhidi ya Liverpool.

West Ham ilikuwa imeshuhudia ushindi mara mbili katika mechi 13 zilizopita.