Michezo

Lengo la Arsenal ni kutinga 4-bora msimu huu – Emery

September 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

KOCHA Unai Emery wa Arsenal amekiri kwamba kikosi chake kimeimarika zaidi kiasi kwamba kitakuwa miongoni mwa wagombeaji halisi wa taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.

“Viwango vya ushindani vimeinuka na kikosi kwa sasa kinatawaliwa na kiu ya kusajili matokeo mazuri katika kila mchuano. Hali ikiendelea kuwa hivi, sioni chochote kitakachotunyima nafasi ndani ya mduara wa nne-bora mwishoni mwa msimu,” akasema Emery ambaye huu ni msimu wake wa pili akidhibiti mikoba ya Arsenal uwanjani Emirates.

Kauli ya Emery ilichochewa na kiwango cha kujituma kwa masogora wake waliotoka nyuma kwa mabao mawili na kuwalazimishia Tottenham Hotspur sare ya 2-2 katika gozi la London Kaskazini lililowakutanisha wikendi iliyopita uwanjani Emirates.

Awali, Tottenham walionyesha dalili zote za kutia kapuni alama tatu katika mchuano huo baada ya kuwazidi maarifa wapinzani wao katika takriban kila idara.

Chini ya mkufunzi Mauricio Pochettino, Spurs walichukua uongozi kupitia kwa kiungo Christian Eriksen kunako dakika ya 10 baada ya kipa Bernd Leno kushindwa kulidhibiti kombora aliloelekezewa na Erik Lamela. Leno alizuia fataki la Son Heung-min kabla ya nyota huyo wa Korea Kusini kukabiliwa visivyo na nahodha Granit Xhaka katika tukio lililomchochea refa Martin Atkinson kuwapa Tottenham mkwaju wa penalti kunako dakika ya 40.

Penalti hiyo iliyofumwa wavuni na Harry Kane ilimwezesha kufikisha jumla ya mabao 10 kutokana na mechi 11 kati ya Arsenal na waajiri wake.

Ufufuo wa Arsenal ulianzishwa na Alexandre Lacazette ambaye alishirikiana vilivyo na sajili mpya Nicolas Pepe na kufunga bao lililowarejesha waajiri wake mchezoni mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Ushirikiano mkubwa kati ya viungo Matteo Guendozi na Dani Ceballos ulimtatiza pakubwa kipa Hugo Lloris ambaye alifanya kazi nyingi ya ziada kabla ya kuzidiwa ujanja na Pierre-Emerick Aubameyang aliyesawazishia Arsenal katika dakika ya 71.

Nusura Kane awape Tottenham bao la tatu katika dakika ya 66 ila kombora lake likabusu mlingoti wa lango la Arsenal ambao walishuhudia bao la beki Sokratis Papastathopoulos likifutiliwa mbali na teknolojia ya VAR kwa madai kwamba alikuwa ameotea.

Matokeo ya mechi hiyo yaliwaweka Arsenal katika nafasi ya tano jedwalini kwa alama saba baada ya mechi nne za ufunguzi wa kampeni za EPL msimu huu. Spurs kwa upande wao wanashikilia nafasi ya tisa kwa alama tano.

Kufikia sasa, Tottenham wameshindwa kujivunia ushindi wowote ugenini kutokana na mechi nane zilizopita ambapo wamelazimishiwa sare mara mbili na kupoteza sita.