Michezo

Lengo ni kubeba taji la wazito Uefa – Kane

May 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MASHIRIKA

MUNICH, Ujerumani

MUDA mfupi baada ya kufungia Bayern Munich bao wakicheza na Real Madrid mnamo Jumanne usiku, mshambuliaji Harry Kane amesema kilichobakia sasa ni kushinda kombe kuu la taaluma yake.

Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Uingereza aliifungia Bayern bao la pili dakika ya 57 katika mechi hiyo ya nusu-fainali iliyomalizika kwa sare ya 2-2, baada ya Leroy Sane kufunga bao la kwanza dakika ya 53.

Madrid ilipata mabao yote kupitia kwa Vincius Junior dakika za 24 na 83.

Timu hizo zitarudiana Mei 8, 2024, ambapo mshindi atacheza fainali dhidi ya timu itakayoshinda kati ya PSG na Borussia Dortmund.

Kane ni mshambuliaji matata, lakini licha ya kusaidia Tottenham Hotspur kung’ara katika Ligi Kuu ya Uingereza kwa miaka mingi, hakuwahi kusaidia timu hiyo kutwaa taji lolote kuu.

Nyumbani katika Ligi Kuu ya Uingereza (Bundesliga), Bayer Leverkusen imezima rekodi ya Bayern ya miaka 11 mfululizo kushinda ligi hiyo, lakini huenda Kane akamaliza kiu yake na kutimiza ndoto hiyo kwa kusaidia Bayern kutwaa ubingwa wa UEFA.

Uhamisho

“Msimu umekuwa mzuri kufikia sasa,” alisema Kane aliyejiunga na Bayern akitokea Spurs kwa kitita cha Sh8.6 bilioni msimu uliopita.

“Sote kikosini tunapigania ubingwa wa Uefa. Si kazi rahisi. Tunatarajia kuenda Bernabeu kwa mkondo wa pili tukiwa na imani ya kutosha. Nimecheza soka kwa muda mrefu. Bila shaka mwanzoni mwa msimu matarajio yalikuwa kushinda ligi. Taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) ndilo kubwa kuliko yote. Iwapo tutafaulu kulibeba, utakuwa msimu wa ajabu. Nilikuja hapa ili nicheze katika mashindano haya makubwa.”

Bao lake alilofunga kutokana na mkwaju wa penalti lilimfanya kumfikia Kylian Mbappe ambaye pia amefunga mabao matano katika michuano ya Ulaya msimu huu.

Lakini anajivunia mabao mengi ya pamoja na ya msaada kuliko mchezaji yeyote kwenye ligi kuu barani ulaya (mabao 43 na 11 ya kuchangia).

Kila mtu ameridhika na mabao yote aliyofunga straika huyo mwenye umri wa miaka 30, huku mchango wake ukifurahisha kila mtu aliyemshuhudia msimu huu.

Akizungumza kuhusu hali yake, kiungo mstaafu Mwingereza, Owen Hargreaves alisema: “Kane alikuja hapa kushinda mataji. Watu wanasema hajashinda lolote, lakini huenda akasaidia Bayern kutwaa ubingwa wa Uefa mwaka huu 2024.”

Kiungo wa zamani wa Real Madrid na timu ya taifa ya Uingereza, Steve Mcmanaman aliongeza: “Kipaji chake hakina ubishi. Akiwa katika hali njema, daima anapata malengo yake.”

Wakati akichezea Bayern, Mwingereza mwenzake, Jude Bellingham alisakatia kikosi cha Real Madrid, na wote wataongoza vikosi vyao katika mechi ya marudiano juma lijalo.