Michezo

Leopards yazuru Sofapaka ikinuia kukwaruza tena

February 22nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

JEFF KINYANJUI na JOHN ASHIHUNDU

SOFAPAKA wamejipanga kulipiza kisasi cha kulimwa katika mkondo wa kwanza na AFC Leopards katika mechi ya Ligi Kuu ya Kenya (KPL) uwanjani Mumias Complex, leo Jumamosi alasiri.

Sofapaka almaarufu ‘Batoto ba Mungu’, chini ya kocha John Baraza walilimwa 2-1 mikononi mwa Ingwe katika duru ya kwanza.

Hata hivyo, walokole hao wataingia uwanjani wakijivunia ushindi wa majuzi wa 3-1 dhidi ya mabingwa watetezi, Gor Mahia.

“Ushindi dhidi ya Gor Mahia ni historia sasa. Kesho (leo Jumamosi) tunacheza na timu tofauti na lazima tucheze kulingana na jinsi tulivyojiandaa wiki hii huku tukilenga ushindi. Tumejiandaa vyema na tunaamini tunaweza kupata pointi zote tatu,” alisema Baraza japo alionya wachezaji wake wasiidharau Ingwe.

Akaongeza: “Ningependa kuwasihi wachezaji wasahau matokeo ya juzi dhidi ya Gor na waelekeze mawazo yao kwa mechi hii. Kawaida inakuwa kazi ngumu kucheza na AFC Leopards ama Gor Mahia kwa sababu ndizo timu kubwa zenye mashabiki wengi nchini.”

Leopards wamepiga kambi mjini Mumias juma hili chini ya kocha wao, Anthony Modo Kimani anayeamini vijana wake wana uwezo mkubwa wa kuibwaga Sofapaka.

Hata hivyo, Kimani ataunda kikosi chake bila Vincent Oburu, Collins Shichenje na Marvin Nabwire ambao wanauguza majeraha.

“Kila tunapochezea Mumias mashabiki wanatupa sapoti ya kutosha na tumejiandaa vyema kwa mechi hii. Kambi ya pamoja imetusaidia na kila mtua ako tayari kupambana hadi dakika ya mwisho,” aliongeza.

AFC Leopards ambao wamezuiliwa kuchezea katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo kutokana na deni la Sh2 milioni walizotozwa kwa uharibifu uliotokea uwanjani humo wakicheza na Gor Mahia, wametegemea michango ya mashabiki kugharimia kambi ya Mumias.

Licha ya matatizo ya kifedha yanayowakabili, Ingwe wamekuwa wakicheza soka ya kiwango cha juu, huku wakipata matokeo mseto. Walikuwa wakijivunia ushindi mara tatu mfululizo kabla ya kushindwa 1-0 na Tusker mjini Nakuru.

“Nimezungumza na vijana kuwasihi wavumilie shida zinazotukumba. Kumbuka wengi wao ni wachanga, na wanazidi kuelewana jinsi tunavyozidi kukaa pamoja,” alisema.

Katika mechi nyingine ya leo alasiri, Bandari watakuwa wenyeji wa Mathare United mjini Mombasa huku Posta Rangers wakivaana na KCB mjini Machakos wakati Western Stima wakikabiliana na Kariobangi Sharks mjini Kisumu.

Ni pointi tatu pekee zinazoitenganisha Tusker na vinara Gor Mahia, lakini vijana hao wa Robert Matano watakutana na Wazito kesho katika kampeni yao ya kuwania ubingwa ambao waliushinda kwa mara ya mwisho mnamo 2012.

Huenda Matano akakosa huduma za mshambuliaji tegemeo Timothy Otieno anayesumbuliwa na jeraha dogo kwenye goti lake.

Ratiba ya mechi za leo Jumamosi ni: Bandari na Mathare United (Mbaraki, saa nane), Posta Rangers na KCB (Machakos, saa tisa), Western Stima na Kariobangi Sharks (Kisumu, saa tisa), AFC Leopards na Sofapaka (saa kumi).

Jumapili: Ulinzi Stars na Kisumu AllStars (Nakuru, saa tisa), Kakamega Homeboyz na Chemelil Sugar (Bukhungu, saa tisa), Tusker na Wazito (Ruaraka, saa tisa), Zoo na Gor Mahia (Kericho, saa nane na robo).