Michezo

Leroy Sane aagana na Manchester City, ayoyomea Bayern Munich

July 1st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

KLABU ya Manchester City imekiri kwamba itamsajili kiungo na nahodha wa Aston Villa, Jack Grealish, kwa matarajio kwamba atakuwa kizibo kamili cha Leroy Sane ambaye ameagana nao rasmi.

Man-City wamefikia maamuzi ya kumuuza Sane ambaye kwa sasa atayoyomea Ujerumani kuvalia jezi za Bayern Munich kwa takriban Sh6.3 bilioni huku kiasi hicho cha fedha kikitarajiwa kuongezeka hadi Sh7.7 bilioni iwapo Bayern watatinga fainali ya kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu.

Sane, 24, aliingia katika sajili rasmi ya Man-City mnamo 2016 baada ya kuagana na Schalke 04 ya Ujerumani kwa kima cha Sh5 bilioni.

Tangu wakati huo, Sane amewaongoza Man-City kutia kapuni mataji mawili ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Sane ambaye kwa sasa atalipwa mshahara wa Sh2.8 bilioni kwa mwaka kambini mwa Bayern, alikuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Man-City kilichotia kapuni mataji matatu kwa mkupuo msimu uliopita.

Hata hivyo, amesalia mkekani kwa takriban msimu huu mzima wa 2019-20 kufuatia jeraha baya la goti alilolipata mwanzoni mwa muhula katika mechi ya Community Shield dhidi ya Liverpool.

Mnamo Juni 27, 2020, kocha Pep Guardiola alisema kwamba Sane ambaye mkataba wake na sasa na Man-City unatarajiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu ujao, alikuwa amekataa kurefusha muda wa kuhudumu kwake uwanjani Etihad na alikuwa amewasilisha ombi la kutaka kuachiliwa kujiunga na Bayern.

Sane anatazamiwa sasa kuyoyomea Ujerumani chini ya kipindi cha saa 24 zijazo ili kurasimisha uhamisho wake hadi Bayern waliotawazwa mabingwa wa soka ya Bundesliga msimu huu.

Ingawa hawezi kuchezea Bayern katika kipute cha UEFA msimu huu, Sane hatarejea tena kambini mwa Man-City na ina maana kwamba gozi dhidi ya Burnley mnamo Juni 22, 2020 ndio uliokuwa mchuano wake wa mwisho ndani ya jezi za Man-City. Sane aliwajibishwa kwa dakika 11 za mwisho wa kipindi cha pili katika mechi hiyo ya EPL.

Japo Guardiola amefichua haja ya kumsajili Grealish ambaye pia anawaniwa na Man-United, Man-City wameshikilia kwamba uwepo wa viungo Phil Foden, Riyad Mahrez, Bernardo Silva na Raheem Sterling bado utawasaza kuwa thabiti na imara zaidi.

Sane anaondoka ugani Etihad akijivunia kuchezea Man-City katika jumla ya mechi 192 na kufunga mabao 52.

Kubwa zaidi ambalo linamwaminisha Guardiola kwamba watajinasia maarifa ya Grealish ni hali tete ya sasa ya Villa kwenye kampeni za EPL huku wakikodolea jicho hatari ya kushushwa ngazi mwishoni mwa muhula huu.