Leroy Sane sasa mali rasmi ya Bayern Munich
Na CHRIS ADUNGO
MJERUMANI Leroy Sane amesema kwamba Bayern Munich ni “kikosi cha haiba kilicho na malengo makubwa katika ulingo wa soka”.
Hii ni baada ya kiungo huyo wa zamani wa Manchester City kutia saini mkataba wa miaka mitano na miamba hao wa soka ya Ujerumani.
Sane, 24, alirasimisha uhamisho wake kutoka Man-City hadi Bayern kwa kima cha Sh6.2 bilioni ila kiasi hicho cha fedha kinatazamiwa kufikia Sh7.6 bilioni iwapo Bayern watatinga fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu.
Sane alijiunga na Man-City kutoka Schalke 04 ya Ujerumani mnamo 2016 kwa kima cha Sh5.1 bilioni. Akiwa uwanjani Etihad, Sane aliwasaidia Man-City kutia kapuni mataji mawili ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Kombe la FA na mataji mawili ya League Cup.
“Natamani sana kunyakua mataji mengi iwezekanavyo nikiwa ndani ya sare za Bayern na kubwa zaidi katika matamanio yangu hayo ni kuwaongoza kutwaa ufalme wa UEFA haraka iwezekanavyo,” akasema Sane.
Sane alikuwa sehemu muhimu ya kampeni za Man-City msimu wa 2018-19 na akasaidia kikosi hicho kutia kapuni jumla ya mataji matatu kwa mkupuo. Ingawa hivyo, jeraha lilimweka mkekani kwa kipindi kirefu msimu huu na hadi kuondoka kwake, alikuwa amechezea kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola mara mbili pekee.
Katika jumla ya mechi 135 ambazo Sane aliwawasakatia Man-City, alifunga jumla ya mabao 39 na kuchangia mengine 45.
“Lengo letu ni kuwaleta pamoja wanasoka bora zaidi duniani kambini mwa Bayern. Ujio wa Sane ni mwanzo wa safari hiyo,” akasema Afisa Mkuu wa Bayern, Karl-Heinz Rummenigge.
Sane ambaye anajivunia kuchezea timu ya taifa ya Ujerumani mara 21, anatarajiwa kuanza mazoezi kambini mwa Bayern wiki ijayo japo hawezi kuvalia jezi za kikosi hicho cha kocha Hansi Flick katika kipute cha UEFA msimu huu.