Michezo

Leteni sasa huyo Tyson Fury – Anthony Joshua

December 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

MWANAMASUMBWI raia wa Uingereza mwenye asili ya Nigeria, Anthony Oluwafemi Olaseni Joshua, 31, amesema yuko tayari kuvaana na mshikilizi wa taji la WBC, Tyson Fury, katika pigano kubwa la kihistoria ambalo sasa maandalizi yake yameanza kushika kasi nchini Uingereza.

Hii ni baada ya Joshua ambaye ni bingwa wa mataji ya WBA, WBO, IBF na IBO kufaulu kutetea ufalme wake mnamo Disemba 12, 2020 kwa kumdengua Kubrat Pulev wa Bulgaria kwa njia ya Knockout (KO) kwenye raundi ya tisa katika pambano la uzani wa juu mbele ya mashabiki 1,000. Mchapano huo ulifanyika katika ukumbi wa SSE Arena, uwanjani Wembley, jijini London, Uingereza.

Kwa mujibu wa Eddie Hearn ambaye ni promota wa Joshua, juhudi za kufanikisha pigano kati ya bondia huyo na Fury zinaendelea.

“Ndilo pigano la pekee katika ulingo wa ndondi ambalo kwa sasa lina ulazima wa kufanyika. Litakuwa pigano kubwa na lenye historia ya kipekee nchini Uingereza na duniani kote,” akasema.

Kauli ya Fearn imeungwa mkono na promota wa Fury, Bob Arum ambaye ameshikilia kwamba kukutana kwa Joshua na mteja wake kutarejesha kumbukumbu za 1971 ambapo Muhammad Ali alivaana na Joe Frazier kwenye mchapano wa karne lililoshuhudia Ali akitwaa ushindi baada ya raundi 12.

“Bingwa yeyote aliye na azma ya kuvaana nami katika ulingo wa ndondi yuko radhi kufanya hivyo. Iwapo huyo atakuwa Fury, basi acha iwe Tyson Fury,” akasema Joshua.

Fury ambaye pia ni Mwingereza, alitumia mtandao wake wa kijamii kumjibu Joshua haraka kwa kuandika, “Natamani sana hilo pigano lijalo. Nitamdengua Joshua kwa Knock-Out baada ya raundi tatu pekee.”

Baada ya kushinda pambano la 25 kati ya 26 aliyoshiriki awali, akiwa ameshindwa mara moja pekee, Joshua amesema ana kiu ya kupanda ulingoni na hawezi akasubiri zaidi kupigana na Fury katika pambano kubwa la kuunganisha mataji.

Joshua alikuwa akichapana Disemba 12 kwa mara ya kwanza tangu arejeshe mataji yake hayo nchini Saudi Arabia mnamo Disemba 2019 kwa kumshinda mwanamasumbwi Andy Ruiz Jr wa Mexico kwa wingi wa alama na kulipiza kisasi cha Juni 2019 jijini New York, Amerika.

Kwa upande wake, pigano la Disemba 12 lilikuwa la pili kwa Pulev, 39, kupoteza kati ya 29 yaliyopita baada ya kuzidiwa maarifa na Wladimir Klitschko kwa mara ya kwanza mnamo 2014.

Ushindi wa Joshua aliyefaulu kuhifadhi taji lake la bingwa wa uzani wa juu zaidi dunia kwa mara ya tatu, ulisherehekewa pakubwa na mamilioni ya watu hasa Magharibi wa mji wa Sagamu, Nigeria inakotokea familia ya bondia huyo.

“Nilijua Pulev alivyo. Nilimsoma mapema. Aliingia ulingoni akidhani kwamba yeye ni shujaa japo alinitatiza katika raundi ya tatu,” akatanguliza Joshua.

“Nilikuwa nimemwambia mara kadhaa asitumie rekodi za ufanisi wa awali kujitapa kwa sababu mimi si sawa na hao aliowadhalilisha hapo zamani,” akaongeza.

Pulev alishuka ulingoni akiwa na uzani wa 239.7lbs (kilo 108.7) baada ya kupunguza uzani wa 9lbs (kilo 4.08) tangu ashiriki pigano lake la mwisho. Kwa upande wake, Joshua alikuwa ameongeza uzani wa 4lbs (kilo 1.81) kutoka kwa 240.8lbs (kilo 109.2) alizokuwa nazo mara ya mwisho alipochapana na Ruiz Jr mnamo Disemba 2019 nchini Saudi Arabia.

Awali, Joshua na Pulev walikuwa wameratibiwa kuchapana makonde katika uwanja wa Tottenham Hotspur jijini London, Uingereza mnamo Juni 20 mwaka huu, kabla ya mchapano huo kuahirishwa kwa sababu ya corona.

Pigano hilo halikufanyika tena Oktoba 2019 uwanjani Cardiff Principality, Uingereza baada ya Pulev kujiondoa katika dakika za mwisho kutokana na jeraha baya la bega.

Pulev alikuwa akiwania fursa ya kutwaa taji la IBF kutoka kwa Joshua ambaye pia ni mshikilizi wa mataji ya dunia ya WBA na WBO.