Michezo

Lewandowski atawazwa Mchezaji Bora Duniani huku Klopp, Neuer, Son na Rashford nao wakituzwa

December 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI Robert Lewandowski wa Bayern Munich alitawazwa Mchezaji Bora wa Kiume wa Mwaka 2020 kwenye tuzo za Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) zilizotolewa jijini Zurich, Uswisi mnamo Alhamisi.

Lewandowski alimpiku mshindi wa tuzo hiyo katika mwaka wa 2019 Lionel Messi pamoja na nyota wa Juventus na timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo.

Lewandowski ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya Poland alifunga mabao 55 kutokana na mechi 47 za msimu uliopita wa 2019-20 na kusaidia Bayern kutia kapuni mataji matatu kwa mkupuo.

Sogora huyo mwenye umri wa miaka 32 pia alikamilisha kampeni za msimu wa 2019-20 akiwa mfungaji bora katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga), mashindano ya kuwania makombe mbalimbali na gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Beki Lucy Bronze wa Manchester City alitawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka kwa upande wa wanawake.

Washindi wa tuzo hizo waliamuliwa kupitia uteuzi uliofanywa na manahodha wa timu za taifa, makocha wa timu za taifa, kura za siri zilizopigwa na baadhi ya mashabiki na wawakilishi 200 wa vyombo vya habari.

Hii ni mara ya kwanza kwa Lewandowski kutia kapuni taji hilo ambalo limekuwa likitamalakiwa na Messi wa Barcelona na Ronaldo.

Msimu huu, Lewandowski amepania kuendeleza ubabe wa msimu uliopita wa 2020-21 na tayari amefungia Bayern jumla ya mabao 16 kutokana na mechi 14 za hadi kufikia sasa msimu huu.

“Iwapo utashinda taji la kiwango hiki na utiwe kwenye tapo moja na Messi na Ronaldo, basi hilo ni jambo lisiloaminika kabisa kwa kuwa lina maana kubwa sana kwangu,” akasema Lewandowski.

“Miaka mingi iliyopita, nakumbuka nilivyowania fursa za kutwaa taji hili. Ni kitulizo kikubwa kwamba hatimaye ndoto hiyo imetimia. Hii ina maana kwamba haijalishi unakotokea mradi tu ujitahidi katika hicho unachokifanya,” akaongeza.

Kwa upande wa makocha, Jurgen Klopp alitawazwa Kocha Bora wa Mwaka kwa ufanisi wa kuwaongoza Liverpool kutwaa taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 mnamo 2019-20. Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Klopp ambaye ni raia wa Ujerumani kupokezwa tuzo hiyo.

Klopp alipokezwa taji hilo mnamo 2019 baada ya kuwaongoza waajiri wake Liverpool kutia kapuni ufalme wa UEFA. Mwaka huu, kocha huyo wa zamani wa Borussia Dortmund aliwabwaga wakufunzi Hansi Flick wa Bayern na Marcelo Bielsa anayedhibiti mikoba ya kikosi cha Leeds United kwenye EPL.

Manuel Neuer wa Bayern alitawazwa Kipa Bora wa Mwaka baada ya kuwapiga kumbo Jan Oblak wa Atletico Madrid na Alisson Becker wa Liverpool.

Kipa huyo raia wa Ujerumani alifungwa mabao 31 pekee katika jumla ya mechi 33 zilizosakatwa na Bayern kwenye Bundesliga mnamo 2019-20 na akategemewa pakubwa kupangua makombora mazito ya wapinzani wao kwenye hatua za mwondoano za UEFA na hatimaye kutwaa ubingwa kwa kupiga Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa 1-0 kwenye fainali iliyoandaliwa jijini Lisbon, Ureno.

Fowadi mahiri wa Tottenham Hotspur, Son Heung-min alituzwa taji la Puskas kwa ubora wa bao lililotokana na juhudi zake dhidi ya Burnley mnamo 2019.

Son ambaye ni raia wa Korea Kusini, alikimbia kutoka kwenye kijisanduku cha Tottenham hadi cha Burnley huku akiwaacha hoi mabeki wote wa timu pinzani na kupachika wavuni bao hilo.

Tuzo hiyo iliyonyakuliwa na Son ilianzishwa mnamo 2009 na kupagazwa jina la fowadi wa zamani wa Real Madrid, Ferenc Puskas.

Wanasoka watatu wa Liverpool waliotwaa taji la EPL mnamo 2019-20 walijumuishwa kwenye kikosi bora cha wachezaji 11 duniani. Hao ni kipa Alisson Becker na madifenda Trent Alexander-Arnold na Virgil van Dijk.

Sajili mpya wa Liverpool, Thiago Alcantara, aliyeagana na Bayern alijumuishwa pia kwenye kikosi hicho kwa pamoja na Kevin De Bruyne wa Manchester City kwenye safu ya kati. Lewandowski aliungana na Messi pamoja na Ronaldo kwenye safu ya uvamizi.

KIKOSI BORA CHA FIFA IX:

Kipa: Alisson (Liverpool)

Mabeki: Trent Alexander-Arnold (Liverpool), Virgil van Dijk (Liverpool), Sergio Ramos (Real Madrid), Alphonso Davies (Bayern Munich).

Viungo: Joshua Kimmich (Bayern Munich), Kevin de Bruyne (Manchester City), Thiago (Liverpool).

Wavamizi: Lionel Messi (Barcelona), Robert Lewandowski (Bayern Munich), Cristiano Ronaldo (Juventus).

Fowadi Marcus Rashford wa Manchester United pia alitambuliwa na kutuzwa kwenye hafla hiyo ya FIFA kwa ukubwa na upekee wa mchango wake katika vita dhidi ya umaskini na ukosefu wa chakula na mahitaji ya msingi miongoni mwa watoto.